Anayedaiwa kupakia mchanga, kuuza kama mbolea na kuvuna Sh209 milioni abanwa kortini
MMILIKI wa kampuni mbili zinazodaiwa kuhusika katika kashfa ya mbolea ya Sh209 milioni kwa kupakia mchanga katika magunia ya mbolea ameshtakiwa.
Josiah Kariuki Kimani alifikishwa katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani mbele ya Bi Celesa Okore.
Kimani alikanusha mashtaka saba ya ufisadi na kuwatapeli wakulima nchini kutokana na mbolea ghushi yenye mchanga.
Kimani ndiye mmiliki wa kampuni za SBL Innovate Manufacturers Limited na African Diatomite Industries Limited zilizopewa kandarasi ya kutengeneza na kusambaza mbolea kwa wakulima.
Mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Renson Igonga alimfungulia mashtaka saba Kimani ya kughushi vyeti vya kutengeneza mbolea akidai vilikuwa vimeidhinishwa na Shirika la Ukadiriaji wa Ubora wa Bidhaa (KeBS).
Alikana kushiriki uhalifu huo mnamo Januari 12, 2023.
Mwekezaji huyo alidaiwa alishirikiana na watu wengine kutoa habari hizo za uwongo kwa maafisa wa KeBS katika afisi zake mjini Nakuru.
Hakimu alielezwa na kiongozi wa mashtaka Bi Everlyn Onunga kwamba Kimani alighushi cheti cha utengenezaji mbolea iliyochanganywa na mabaki ya mifugo akidai kilitayarishwa na kutiwa saini na KeBS.
Kimani alidaiwa kughushi cheti nambari 14617 kilichotolewa kwa kampuni zake kwa majina 51 Capital na African Diatomite K Limited za ubora wa mbolea alizotengeneza.
Bi Onunga alimweleza hakimu Okore kwamba mshtakiwa alipeleka cheti nambari 14617 kwa Halmashauri ya Nafaka na Mazao akidai kampuni zake zilikubaliwa kuwasilisha mbolea ambayo wakulima wangenunua.
Kinara huyo wa kampuni hizo mbili alikabiliwa na shtaka jingine la kupokea cheti nambari 69392 cha kutengeneza mbolea asili ya kiwango cha KS 2290:2018 kinachokubaliwa na KeBS.
Kimani alishtakiwa siku tano baada ya kushtakiwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa NCPB Bw Joseph Muna Kimote kwa kuwauzia wakulima magunia 139,688 ya mbolea ya thamani ya Sh209,532,000.
Bw Kimani aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema Jaji Diana Kavedza wa mahakama kuu ya Kibra alikuwa amemwachilia kwa dhamana ya Sh100,000.
Lakini Bi Onunga alipinga mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana sawa na hiyo ya Jaji Kavedza akidai “kampuni zake ndizo zilihusika na utengenezaji na usambazaji wa mbolea hiyo feki.”
Bi Onunga alisema mshtakiwa hakuwa amefunguliwa mashtaka alipoachiliwa na Jaji Kavedza na “kwamba hali yake imebadilika sasa.”
Hakimu alielezwa kwamba mbolea hiyo ilisababisha mtafaruku mkubwa miongoni mwa Wakenya na washikadau huku Onunga akisema tabia hiyo inaweza kusababisha uhaba wa chakula nchini.
Kimani atashtakiwa pamoja Kimote aliyeshtakiwa Jumatano wiki iliyopita pamoja na John Kiplangat Ngetich (katibu mkuu wa NCPB) na John Mbaya Matiri (meneja mkuu wa uuzaji) kwa kula njama za ulaghai wa Sh209,532,000.
Watatu hawa walishtakiwa kuwapuja wakulima kwa kuwauzia mchanga uliochanganywa na mawe wakidai ni mbolea safi.
Hakimu alifahamishwa kati ya Machi 17, 2022 na Machi 8,2024 washtakiwa hao walikula njama kuwauzia wakulima magunia 139,688 ya mchanga uliokarabatiwa yenye thamani ya Sh209,532,000.
Shtaka lilisema mchanga huo uliokuwa umepakiwa kwa magunia ya kilo 25 ulidaiwa kuwa mbolea halisi.
Kimote, Ng’etich na Matiri walishtakiwa pamoja na Josiah Kariuki Kimani ambaye ni mmiliki wa kampuni mbili Fifty One (K) Capital Limited na SBL Innovate Ltd zilizopewa kandarasi ya kuigiza mbolea nchini.