Hofu yazuka kambi ya Arsenal, Man City ikionyesha ukatili wa kufinya timu zote
JOHN ASHIHUNDU NA MASHIRIKA
BAADA ya mechi zilizochezwa mwishoni mwa wiki, Manchester City wanaendelea kuipa joto Arsenal katika vita vya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2023/2024.
Kwenye mbio hizo, Arsenal wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 83 waliibuka na ushidi wa 3-0 dhidi ya limbukeni Bournemouth, saa chache tu kabla ya City wanaojivunia 82 kucharaza Wolves 5-1, na kuendelea kushikilia nafasi ya pili.
Vita hivi vimekuwepo kwa wiki kadhaa, huku makocha wa timu hizo- Mikel Arteta wa Arsenal na Pep Guardiola wakieleza matumaini yao makubwa.
Baada ya Arsenal kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye London debi, mashabiki wao walifurahia huku wakidhania City watavurugwa na Nottingham Forrest waliokuwa wakiwania kuondoka eneo hatari la kupigwa shoka, lakini mashabiki hao wa The Gunners waliduwazwa na kichapo cha 2-0 ambacho City walipokeza Forrest.
Ni hali iliyowaweka Wanabunduki kwenye masikitiko makubwa wakati mechi iliyofuata Manchester City ilipopokeza Mbwa Mwitu Wolves 5-1 na kuwakaribia kabisa huku vijana hao wa Guardiola wakiwa wangali na mechi moja mkononi.
Itakumbukwa kwamba makocha hao waliwahi kufanya kazi pamoja katika klabu ya Manchester City, na kila mmoja anaelewa mwenzake.
Katika mechi zilizopita, timu zote zimekuwa zikifunga mabao mengi kila moja ikipigania kuipiku nyingine. Arsenal imekuwa na safu imara ambayo imekuwa moja kati ya silaha ya kuendeleza ubabe msimu huu, wakati City wakitegemea safu ya kati na ya ushambuliaji katika juhudi zao za kuwania kuhifadhi ubingwa.
Katika mechi zilizobaki, Arsenal watacheza na Manchester United ugenini kabla ya kualika Everton katika mechi ya mwisho.
Manchester City kwa upande wake wamebakisha mechi tatu dhidi ya Fulham halafu Tottenham Hotspur ugenini kabla ya kualika West Ham nyumbani.
Matokeo ya mechi za wikendi
Brighton 1 Aston Villa 0, Chelsea 5 West Ham United 0, Manchester City 5 Wolves 1, Brentford 0 Fulham 0, Sheffield United 1 Nottingham Forest 3, Burnley 1 Newcastle United 4.