Makala

Wakazi wa Kiambogo wanavyoishi na hofu ya kumezwa na ardhi

May 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA STEVE OTIENO

WAKAZI wa Mukuru Wa Nyatoro, Kiambogo, Kaunti ya Nakuru kwa sasa wanaishi katika mazingira hatari baada ya mashamba yao kuathirika na tetemeko la ardhi na maporomoko ya ardhi.

Hali hiyo imeyaacha mashamba hayo yakiwa na mashimo makubwa na kuzua hatari zaidi hasa wakati huu ambapo mvua kubwa inaendelea kunyesha eneo hilo.

Mwanzoni, ardhi ilianza kuwa na laini ya mipasuko midogo ambayo ilibadilika na kuwa mikubwa. Katika hali hiyo, baadhi ya mimea ambayo walikuwa wamepanda iliharibika nao wakiingiwa na wasiwasi kuhusu usalama wao.

Baada ya kupasuka kwa ardhi hiyo, kuna baadhi ya sehemu ambazo zilianza kutoa mvuke na wakazi wakaingiwa na wasiwasi zaidi.

Mnamo Ijumaa iliyopita, mtaa huo wa Mukuru wa Nyatoro ulishuhudia tetemeko la ardhi na mipasuko huku wakazi wakiyahofia maisha yao.

Wakati wa tukio hilo, hakuna mkazi ambaye alidhubutu kutoka nje ya nyumba yake. Ni siku iliyofuatia ya Jumamosi ndipo walifahamu kile kilichotokea.

Mashimo ambayo yalikuwa madogo yalipanuka na yakawa ya kina kirefu zaidi kisha yakaenea kwa zaidi ya kilomita moja.

Vishindo walivyovisikia usiku na tetemeko la ardhi lilisababisha maporomoka ya ardhi ambayo yalijaza baadhi ya mashimo makubwa.

ilichowashangaza zaidi ni kuwa mashimo ambayo yanatoa mvuke, yanameza maji ya mvua na kubakia yamekauka.

Mkazi Priscilla Nthenya, 69, hajawahi kushuhudia tukio hili la ajabu ila wasiwasi wake ni kuwa baadhi ya mipasuko ya ardhi imeanza kushuhudiwa chini ya nyumba yake.

‘Sijawahi kulala hata siku moja’

“Sijawahi kulala hata usiku mmoja. Huwa naketi tu kochini nikimwomba Mwenyezi Mungu nyumba yangu isimezwe. Sina mahali pa kuenda na huwa ninasikia serikali ikisema tuhame bila kutuambia mahali pa kuenda,” akasema akidondokwa na machozi.

Bi Nthenya ni mama wa watoto wanne na pia ana mjukuu. Anafuga ng’ombe wachache na mbuzi kwenye ekari moja ya shamba lake Kiambogo. Ni mjane na watoto wake wote wapo jijini Nairobi ambapo wameenda kusaka ajira japo bado hawajafanikiwa.

“Kwa nini serikali haichukui hatua zozote kuja kutuokoa. Ni lazima mtu afe au nyumba zetu zimezwe ndipo waje hapa kutusaidia. Tunahitaji msaada sasa,” akaongeza.

Moses Thuo, ambaye ni mkulima hodari, ni jirani yake Bi Nthenya na ardhi ya shamba lake imepasuka sana, hali inayomtia wasiwasi.

Katika shamba hilo, kuna mti ambao unaelekea kuanguka na unakadiriwa umekuwepo kwa zaidi ya miaka 100.

Bw Thuo anakiri kuwa mti huo hatimaye utaanguka lakini hadi anapotembeza Taifa Leo katika shamba lake kuna mvuke ambao bado unatokea sehemu ya mpasuko mkubwa.

“Nimepoteza mali na pesa ambazo niliwekeza katika kilimo hapa kwenye shamba langu. Miwa na migomba ya ndizi imeanguka na hasara inaendelea kushuhudiwa kwa wingi,” akasema Bw Thuo.

“Kwenye hali ya sasa, siwezi kuuza shamba hili hata kama ningetaka kwa sababu hakuna atakayelinunua. Hasara ipo tele,” akaongeza.

Shamba lake la ekari nne sasa limefunikwa na mchanga unaotokana na maporomoko ya ardhi. Pia maji ya mvua yanayoelekea kwenye mashimo makubwa yanapitia shambani humo.

“Tunaishi kwa hofu. Bado tunashangaa nini kinaendelea. Nimeishi hapa tangu 1984 na tumekuwa na maporomoko ya ardhi ila hatujawahi kushuhudia ardhi ikipasuka na sehemu yake kuzama kisha mvuke kutoka. Pia hatujui maji haya yanaenda wapi kwa sababu yanapotea tu punde yanapomezwa shimoni,” akasema.

Japo mvua imekuwa ikinyesha kwa wingi, mzee mmoja wa kijiji cha Kimiricho Nyaikuru, alisema mvua ya mwaka huu imekuwa nyingi mno ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Mzee huyo alikuwa wa kwanza kutembelea eneo hilo na kumwarifu chifu kuhusu hatari iliyopo. Tangu maafisa hao wa utawala watembelee eneo hilo, hakuna chochote ambacho kimefanyika.

Mzee wa kijiji asikitika

Aidha, mzee huyo wa kijiji alimsikitikia Bi Nthenya ambaye ameathiriwa pakubwa na mpasuko wa ardhi uliokata nyumba. Hata hivyo, alisema hawana mali na uwezo wa kumhamisha hadi eneo jingine.

“Hili ni suala ambalo linastahili kuchukuliwa kwa makini. Hii ni kwa sababu mpasuko na maporomoko haya yakiendelea, basi tutapoteza watu wengi hapa,” akasema.

Afisa mmoja wa polisi katika kituo kidogo cha polisi eneo hilo ambaye hakutaka atajwe, alisema ni vyema hakuna maisha ambayo yamepotea na hatua inastahili kuchukulia kuwaondoa wakazi hao kwenye hatari inayowakodolea macho.

Chifu wa eneo hilo hakuwepo afisini mwake wala hakupokea simu kuzungumzia kile ambacho serikali inapanga kufanya ili kuwaokoa watu ambao maisha yao yako hatarini.

Pia hakujibu jumbe ambazo alitumiwa kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hizi. Matukio yanayoshuhudiwa Kiambogo ni kati ya yale ambayo yamekuwa yakiathiri maeneo mengine tangu mvua kubwa ianze kushuhudiwa nchini wiki tatu zilizopita.

Watu wasiopungua 210 wameaga dunia kutokana na mafuriko hayo, familia 33,100 ambazo ni watu 165,500 wakilazimika kuhama makwao na shule 1,967 zikiharibiwa.

Wizara ya Usalama wa Ndani imewataka Wakenya wanaoishi katika maeneo ambayo yapo kwenye hatari ya kuathiriwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi wahame makwao. Hata hivyo, wengi wanalalamika kuwa hawana popote pa kuenda.