Makala

Harusi ya viziwi wawili yasisimua na kuvutia umati mkubwa

May 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MERCY KOSKEI

WANANDOA walio na ulemavu wa kuongea na kusikia kutoka Kaunti ya Nakuru hapo Jumapili walifunga pingu za maisha katika hafla iliyovutia umati mkubwa uliotaka kushuhudia hafla hiyo ya kipekee.

Akiwa amevalia gauni jeupe, Grace Wanjiru, 25, akiwa amesindikizwa na wazazi wake, alitembea kwa fahari hadi kwenye madhabahu ambapo mumewe  Thomas Mmisu Likhodo, 50, alikuwa akimsubiri kwa hamu na tabasamu.

Wapenzi hao walibadilishana viapo vya kimyakimya kwa usaidizi wa wakalimani wa lugha ya ishara katika sherehe ya kupendeza ambayo iliwashangaza wakazi mjini Nakuru.

Wawili hao walifunga ndoa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Francis mjini Nakuru.

Kuanzia viapo hadi hotuba, kila kitu kilifanyika kwa lugha ya ishara ili kuhakikisha kuwa wote waliohudhuria wanafuata shughuli zilivyokuwa zikiendelea.

Grace Wanjiru, 25, akivishana pete na homas Mmisu Likhodo,50, wakati wa harusi yao. Picha|Bonface Mwangi

Baada ya kula viapo vya ndoa, nyuso zao ziliangaza kwa furaha kuashiria furaha yao ya ndani na kuridhika kwa ndoto hiyo.

Wasimamizi, Bi Jenifer Wanja Maina na Bw Bethwel Kinyua pia walikuwa viziwi.

Bi Mary Josephine Adhiambo ambaye alikuwa mfasiri katika harusi hiyo alisema kuwa wawili hao walikutana katika chuo cha Mater Dei ambapo Bi Wanjiru alikuwa akisomea mapishi huku Bw Mmusi alikua amefiak kwa kikao cha ushauri.

Licha ya ulemavu wao wa kusikia na usemi na tofauti zao za umri, wawili hao walianzisha uhusiano na Bw Mmusi angeweza kumtembelea shuleni.

Mnamo Septemba 2023, wawili hao walijitokeza na kumjulisha kwamba walitaka kuoana kanisani. Alianza kuwatayarisha kwa ajili ya ndoa kwa kuwapeleka kwa ushauri kwani wanahitaji kuwa na afya njema ya akili.

“Nilipojua kuwa ni marafiki, nilikaa nao na kuwauliza wana urafiki wa aina gani, niliwauliza ikiwa walikua wanataka kuoana, walinieleza kuwa wanafikiria jambo hilo, nikaanza kuwaandaa na hapa tulipo leo,” alisema.

Kulingana na mamake bi harusi, Bi Mary Wanyoike, alishtuka alipojua kwamba bintiye wa kwanza alikuwa akipanga harusi kanisani.

Alifichua kuwa ni mshtuko kwa familia nzima kwani hawakutarajia binti yao ambaye ana matatizo ya kusikia na kuongea atapata mpenzi na hata kufunga ndoa kanisani.

Bi Wanyoike, mkazi wa Nyandarua alisema kwamba alipokea simu kutoka kwa bintiye mdogo ikimwarifu kuwa Grace alikuwa amekutana na mtu ambaye alitaka kumuoa.

BUSU LA UPENDO: Wawili hao hawakuona haya kuonyesha mapenzi mbele ya hadhira ya watu. Picha|Bonface Mwangi

Alisema kuwa alipuuzilia mbali madai hayo na hata kumwambia kuwa huo ulikuwa uhusiano wa mtandao tu ambao utafika kikomo.

Hata hivyo, miezi kadhaa baadaye alimtembelea bintiye aliyekuwa akisoma Nakuru. Bi Wanjiru alimtambulisha mamake kwa mpenzi wake na mwanamume huyo akamhakikishia kwamba anampenda bintiye na alikuwa na nia ya kumuoa.

Babake bi harusi Bw John Wanyoike hakuweza kuficha furaha yake baada ya bintiye kufunga ndoa. Ilimbidi asafiri kutoka Mombasa kushuhudia sherehe hiyo na kumkabidhi bintiye.

Alisema kuwa Bi Wanjiru alizaliwa na kukulia Kaunti ya Mombasa kabla ya kuhamia Nyandarua 2019 na baadaye Nakuru ambapo alijiunga na chuo cha ufundi.

“Mama yake aliponieleza kuwa binti yetu amepata mtu nilifurahi sana kama baba. Alipotuomba baraka nilikubali. Ni mapenzi ya Mungu,” alisema.

Kwa Bw Likhondo alifikishwa altarini na mdogo wake Elijah Likholo na dada yake mkubwa Bi Margret Ngotio.

Bi Margret alisema kuwa kakake alizaliwa bila ulemavu huo lakini baada ya kufikisha umri wa miaka saba alipata matatizo na kupoteza usemi wake na baadaye akawa kiziwi.

Alisema kuwa kama familia walifurahi alipowafahamisha kuwa amepata mwanamke wa kuoa ambaye pia alikuwa kiziwi.

“Tupo hapa kwa niaba ya wazazi wetu, tumefurahi sana kwa ajili yake atapata kuonja ndoa. Nawasihi tu watembee nyumbani, ili ndugu wengine wakutane naye. Yeye ni mtoto wa sita katika familia yetu. Sijawahi kuelewa kilichotokea hadi alipopata matatizo na akawa kiziwi,” alisema.