Watu wanne waokolewa kutoka kwa vifusi vya ghorofa
NA SAMMY KIMATU
WATU wanne wameokolewa ndani ya jengo la orofa tatu ambalo lilikuwa limebomolewa wakati wa uondoaji wa majengo yaliyo kwenye mkondo wa Mto Ngong katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo, tarafa ya South B, eneobunge la Starehe.
Mkuu wa Polisi eneo la Makadara, Bi Judith Nyongesa, alithibitisha Jumanne kwamba waathiriwa walikuwa wamenaswa ndani ya jengo hilo Jumatatu wa saa tisa za mchana.
Aliongeza kuwa vijana kadhaa walikuwa wakikata vyuma chakavu kutoka kwa minara na nguzo za jengo hilo wakati wa mkasa huo.
Baadhi ya vijana waliosababisha ajali hiyo wanasadikiwa walikuwa katika orofa ya chini wakikata vyuma kutoka kwenye sehemu iliyokuwa chini.
Wakati Taifa Leo iliwasili katika eneo la tukio Jumatatu mwendo wa saa kumi na mbili na nusu jioni, mamia ya wakazi walikuwa wamekusanyika wakifuatilia matukio huku wengine wakisimama juu ya vifusi kwenye ng’ambo ya pili katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kenya Wine.
Ghafla shughuli za uokoaji zilivurugwa na kundi la vijana waliorushia polisi mawe wakidai walikuwa wamechelewa mno kuwahi katika eneo hilo kushughulikia mikasa.
Ilikuwa ni mguu niponye kila mmoja akihofia maisha yake.
Wakati wa vurugu hizo, waliokuwa katika eneo la mkasa ni pamoja na mkuu wa tarafa ya South B, Bw Solomon Muraguri, maafisa wa polisi, machifu na timu ya kukabiliana na masuala ya dharura kutoka Kaunti ya Nairobi.
Waliozungumza walisema kulikuwa vijana zaidi ya 30 waliokuwa kwenye jengo hilo wakishindana kukata vyuma ili wauze kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu.
Aidha Bi Nyongesa alisema mwanamume mmoja aliokolewa Jumatatu jioni kutoka kwa vifusi huku akisema hao wengine wanne walifanikiwa kujiokoa.
“Kwa jumla ni watu watano walioponea kifo. Mmoja aliokolewa Jumatatu mwendo wa saa kumi na mbili jioni. Hakuwa na majeraha yaliyoonekana lakini alipatiwa huduma ya kwanza na yuko salama. Wengine ni wanaume wanne ambao walifanikiwa kujiokoa kutoka kwa vifusi,” Bi Nyongesa akasema.
Vilevile, Bi Nyongesa aliwaomba wananchi kupea polisi nafasi na maafisa wengine wanaohusika kutekeleza agizo la Rais William Ruto kubomoa majengo yote yalio kwenye mkondo wa maji bila kutatiza shughuli hizo.
Kadhalika, aliwaonya wakazi wa Mukuru kukoma kueneza uvumi, propaganda na habari za uongo na ambazo hazijathibitishwa hasa sinazohusiana na vifo.