Gachagua: Uongozi ni sawa na mbwa na siku yake
NA MWANGI MUIRURI
NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewaonya wanaompiga kisiasa kwamba bahati ya mwenzao wasiilalie mlango wazi na kwamba kila mbwa huwa na siku yake ya ufanisi.
“Mimi ndio tu mwenye ujasiri na ukakamavu wa kuongoza huu Mlima. Mkipangiwa halafu muwe mikononi mwa wasaliti mtaangamizwa. Umoja wetu kama jamii ndio ngao yetu,” akasema Bw Gachagua.
Aliwaambia kwamba “endeleeni tu kunipangia na kuhujumu umoja wa Mlima mkitumiwa na mikono kutoka nje”.
“Lakini hawa watu wetu si wajinga. Wanawaona tu na wakati wa maamuzi ndio mtaduwaa,” akasema.
Alisema ajenda zake za kukimbizana na miradi ya maendeleo na sera za kuinua uchumi hasa kilimo, ndio utendakazi wake wa kumnusuru vita hivyo Mlimani.
“Kila mbwa na siku yake. Hivi viti tulivyo navyo kwa sasa sio vyetu. Mnasumbuka sana mkivitaka lakini ni Mungu huvigawa. Atakupa ikiwa amekupangia changu. Kwani wakati sikuwa nacho sikuwa nikila na nikinywa? Kwani kuna anayekula kwa mwingine? Wewe endelea kutafuta viti eti vya 2027 na 2032. Hata nani amekwambia au kukupa hakikisho utakuwa hai wakati huo?” akahoji.