Habari za Kitaifa

Mkurugenzi ashtakiwa kutumia stampu ya wakili aliyekufa kufanya mapinduzi

May 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa kampuni moja ya majanichai Kaunti ya Murang’a ameshtakiwa kwa kughushi stampu na saini ya wakili aliyekufa miaka 11 iliyopita kuwatimua uongozini wakuregenzi wenzake wanne.

Bw Kirubi Kamau aliyeshtakiwa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani Geoffrey Onsarigo alikana kughushi stampu na saini ya wakili Mburu Mbugua aliyeaga dunia mnamo Desemba 2008.

Bw Kamau amekana alitumia stampu na saini ya marehemu kuwasilisha ripoti katika Ofisi ya Msajili wa Kampuni mnamo Juni 11, 2019.

Bw Kamau amekana kughushi stampu na saini ya Mbugua katika afidaviti iliyothibitisha Mabw Meshack Kibunja Kaburi, Daniel Wanjie Waruingi, James Njukia Ihura na David Macharia Gichure wamejiuzulu kuwa wakurugenzi katika kampuni ya Central Highland Tea Company Limited.

Akitoa ushahidi, afisa wa uchunguzi wa jinai Konstebo Schola Mwaura alimweleza Bw Onsarigo kwamba Bw Kamau alighushi saini na stampu ya wakili Mbugua ambaye ofisi yake ilikuwa katika jumba la Uganda House.

Konstebo Mwaura alimpa hakimu cheti cha kifo cha Mbugua pamoja na tangazo la kifo chake lililochapishwa na gazeti la Daily Nation.

Afisa huyo kutoka kitengo cha Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) katika kituo cha polisi cha Central alimweleza Bw Onsarigo kwamba wakurugenzi hao wanne walipigwa na butwaa kugudua kwamba wamejiuzulu nyadhifa zao katika kampuni hiyo ya majanichai.

Hakimu alielezwa ripoti iliwasilishwa kwa polisi ilipotambuliwa kwamba wakili aliyekufa Desemba 2008 na kuzikwa miaka minane iliyopita (2019) ndiye alitia sahihi afidaviti zao za kujiuzulu kama wakurugenzi wa kampuni hiyo ya majani chai.

Konstebo Mwaura alifululiza hadi ofisi ya Mwanasheria Mkuu na kubaini kwamba ripoti ya mabadiliko katika uongozi wa kampuni hiyo iliwasilishwa Juni 11, 2019, na Bw Kamau.

Pia alimweleza hakimu kwamba Bw Kamau alitia saini rekodi ya mabadiliko katika uongozi wa kampuni hiyo ya chai.

Hakimu alielezwa saini katika afidaiti hizo za kujiuzulu kwa Mabw Meshack Kibunja Kaburi, Daniel Wanjie Waruingi, James Njukia Ihura na David Macharia Gichure zilikuwa feki.

Mahakama ilielezwa mtaalamu wa masuala ya maandishi alithibitisha kwamba saini za wakurugenzi hao katika afidaviti za kujiuzulu zilikuwa feki.

Afisa huyo wa uchunguzi pia alimweleza hakimu kwamba barua zilizoambatana na afidaviti hizo za kujiuzulu zilikuwa feki.

Konstebo Mwaura aliongeza kuambia mahakama kwamba Chama cha Wanasheria nchini LSK kilithibitisha kwamba marehemu (Bw Mbugua) hakuwa amemteua wakili yeyote kuendeleza shughuli za ofisi yake wakati hayuko.

Konstebo Mwaura alikana madai ya Bw Kamau kwamba alimshtaki kwa sababu ya chuki.

“Umemshtaki Bw Kamau kwa sababu ya chuki na husuda,” wakili wa mshtakiwa alimwelekezea Konstebo Mwaura.

Akijibu Konstebo Mwaura alisema: “Nilimkamata mshtakiwa na kumshtaki kwa sababu ya kufuata haki. Alighushi saini na stampu ya wakili aliyekufa kupotosha Ofisi ya Msajili wa Kampuni.”

Bw Kamau atajitetea mnamo Juni 6, 2024.

Yuko nje kwa dhamana.