Bambika

Pasta Kanyari aitwa na KFCB kufunzwa kutumia TikTok

May 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA FRIDAH OKACHI

MHUBIRI wa kanisa la Salvation Healing Pasta Victor Kanyari ambaye anazingirwa na utata kufuatia matamshi yake na vitendo vilivyoibua shutuma nyingi kwenye mtandao wa TikTok, Ijumaa alishiriki kikao maalum na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Udhibiti wa Filamu nchini (KFCB), Dkt Ezekiel Mutua.

Kikao hicho kilihusu kupata mafunzo ya ushauri. Dkt Mutua alifichua kuwa Pasta Kanyari alianza kupokea mafunzo kufuatia matendo yake.

“Nipo hapa na Mchungaji Kanyari. Tumeanza mafunzo ya ushauri,” alisema Bw Ezekiel Mutua.

Mkutano huo unajiri wakati ambapo pasta huyo mwenye utata amekuwa akipokea shutuma nyingi kutoka kwa wanamtandao kufuatia matendo yake ya hivi majuzi.

Wakati wa mkutano huo, Bw Ezekiel Mutua, alichukua fursa ya kumwombea pasta huyo huku akiwa amepiga magoti mbele yake. Siku ya Alhamisi, Bw Kanyari aliomba msamaha Wakenya baada ya kupokea zawadi kutoka kwa shabiki wake ambaye alimpa pakiti ya kondomu kwenye madhabahu ya kanisa lake.

Hii ikiwa ni mojawapo ya video ambayo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikimpaka tope pasta huyo ambaye kwa wakati mwingi amekuwa akizungumza kwenye mtandao wa TikTok bila breki.

“Msichana kutoka ukambani aliniletea kondomu katika madhabahu. Sikujua, mimi nimefanyia Mungu kazi kwa miaka 30 na sijawahi ona mtu ambaye anaweza kuleta vitu kama hivi katika madhabahu,” alisema Kanyari.

“Hakuna mtu hakoseagi, msichana huyo alikosea na mimi pia sikutaka kumpiga maana ningeongea angepigwa na washirika,” alijitetea Kanyari.

Alisema mwanadada huyo alikuwa mwanatiktok ambaye alimuona mhubiri huyo kwenye mtandao huo wa kijamii na kuamua kutembelea kanisa lake.

Mapema wiki hii, Dkt Ezekiel Mutua alikuwa amejitokeza akizungumzia kuhusu kasisi huyo akidai kuwa angetoa taarifa ambayo ingemfanya apigwe marufuku kutoka kwa TikTok na afungwe jela.

Alidai kuwa Pasta Kanyari alikuwa akidhalilisha jina la upasta na pia makasisi wote nchini.