Dimba

Xavi aenda na maji: Barcelona yamtema kocha kama chingamu

May 25th, 2024 1 min read

NA CECIL ODONGO

BARCELONA Ijumaa ilipiga abautani na kumfuta kazi Kocha Xavi Hernandez.

“FC Barcelona ingependa kumshukuru Xavi kutokana na kazi aliyoifanya kama kocha, mchezaji wa zamani na pia nahodha. Inamtakia kila la kheri katika kazi yake ya ukufunzi,” ikasema taarifa ya Barcelona Ijumaa.

Xavi atasimamia mechi ya mwisho ya msimu kati ya Barcelona na Sevilla Jumapili.

Mwezi Aprili, Xavi alikubali kukamilisha mkataba wake Camp Nou hadi Juni 2025.

Ni uamuzi uliokujia baada ya wakuu wa Barca kumbembeleza asiondoke, baada ya kocha huyo mnamo Januari kutangaza kuwa angeagana nao mwishoni mwa msimu huu.

Ulikuwa wakati alizidiwa na presha kali kutokana na kikosi hicho kusajili matokeo duni.

Hata hivyo, Rais wa Barcelona, Joan Laporta, alimsihi na hatimaye kumshawishi asalie nao ila sasa wamemfuta.

Xavi amekuwa Barcelona kwa miaka mitatu japo msimu huu timu hiyo imetoka kavu kavu ikikosa kushinda Ligi Kuu (La Liga), Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wala Kombe la Uhispania (Copa del Rey).

Barca tayari ipo katika hatua za mwisho za kuafikiana na kocha wa zamani wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Hansi Flick, ili achukue nafasi ya Xavi.

Inasemekana kilichomchongea Xavi ni kauli yake kuelekea mechi dhidi ya Almeria wikendi iliyopita, ambapo alisema Barcelona imesota na inahitaji kujikwamua kiuchumi ili kushindana na mahasimu wao wakuu Real Madrid.

Xavi alieleza kwamba hali imekuwa tete klabuni humo kifedha na kocha hawezi kumnunua mwanasoka yeyote ambaye angependa jinsi ilivyokuwa miaka 25 iliyopita.

Alikariri kuwa atasaidia klabu hiyo kupigania mataji lakini hali yao ya kifedha lazima iimarike haraka ili wanunue wachezaji wa haiba kama Real Madrid ambao wapo sawa kifedha.

Barca wako nyuma ya Real alama 14 ikibaki mechi moja ligi itamatike.

Xavi alichukua usukani Novemba 2021 akitokea klabu ya Saudia ya Al Sadd, na akaongoza Barca kushinda La Liga msimu 2022-23.