Habari za Kaunti

Hoteli za Bungoma zafurika wateja Madaraka Dei ikibisha hodi

May 25th, 2024 2 min read

NA JESSE CHENGE

HOTELI na maeneo ya burudani katika Kaunti ya Bungoma zimeanza kujaa huku wageni kutoka sehemu mbalimbali za nchi wakiwasili kwa Maonyesho ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Kibabii kilichoko eneo la Kanduyi, Kaunti ya Bungoma.

Matarajio ni makubwa huku kaunti hiyo ikijiandaa kwa Maadhimisho ya Madaraka Dei mnamo Juni 1, 2024.

“Kaunti ya Bungoma iko tayari kuandaa Maonyesho ya Kilimo na kuwapokea wageni kutoka mbali na karibu kushiriki katika kuonyesha uwezo wa kilimo katika eneo letu,” alisema Gavana wa Bungoma Ken Lusaka, akisisitiza umuhimu wa tukio hilo.

Idadi kubwa ya wageni katika Kaunti ya Bungoma imesababisha hoteli katika eneo hilo kufurika wateja huku bei za vyumba zikipanda maradufu.

“Mahitaji ya malazi yanaonyesha ahadi ya kiuchumi ya kaunti yetu na msisimko unaohusiana na Maonyesho ya Kilimo,” alisema Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kibabii Prof Odeo Ipara.

Meneja wa hoteli ya Siritamu, Bw Kepha Areba, alisema biashara imenoga.

“Wateja wamefurika pomoni kutokana na wageni wanaohudhuria Maonyesho ya Kilimo na sherehe za Madaraka Dei zinazotarajiwa,” alisema Bw Areba.

Mwenzake wa Sawan Hotel, Bw David Mugo alisema hoteli zinafikia uwezo kamili huku wageni kutoka sehemu mbalimbali za nchi wakihitaji malazi wakati huu wenye shughuli nyingi na za kusisimua kabla ya maadhimisho ya siku ya Madaraka.

Licha ya changamoto katika sekta ya kilimo, Kaunti ya Bungoma bado inaendelea kuwa kitovu cha shughuli za kilimo kwa sababu ya ardhi yake yenye rutuba na mito ya kutoa maji.

Mkulima mmoja alisema lengo ni “kuonyesha uwezo wa sekta ya kilimo katika eneo letu na kushirikiana na kaunti nyingine kwa ajili ya ukuaji wa pamoja.

Naibu Rais Rigathi Gachagua na maafisa wengine, wanatarajiwa kuhudhuria Maonyesho ya Kilimo.

Aidha kilele kitakuwa ni Madaraka Dei ambapo Rais William Ruto ataongoza taifa kwa sherehe za kitaifa.

Maonyesho ya kijeshi yatakayoongozwa na Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Charles Kahariri katika Uwanja wa Masinde Muliro huko Kanduyi yanatarajiwa kuongeza uchangamfu wa kitaifa katika Madaraka Dei.

“Tunatarajia maonyesho ya kijeshi na kisha hotuba ya Rais Ruto huku tukiadhimisha uhuru wetu,” alisema Bw Eric Wekesa, ambaye ni mkazi wa Bungoma.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) mwaka 2019 Bungoma ilikuwa na jumla ya watu 1,670,570, ambapo asilimia 49 ni wa jinsia ya kiume huku 51 ikiwa ni jinsia ya kike.