Habari za Kitaifa

Matabibu walaumiwa mtoto kukatwa mkono

May 25th, 2024 2 min read

NA MARY WANGARI

UTEPETEVU wa daktari wa zamu na ukosefu wa mashine za CT Scan katika hospitali mbili, ni miongoni mwa matukio yaliyosababisha mtoto mchanga kukatwa mkono wake, siku chache tu baada ya kuzaliwa, Seneti imeelezwa.

Kamati ya Seneti kuhusu Afya imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo mtoto Jennifer Mwasi alipoteza mkono wake wa kulia uliokuwa umeanza kuoza kutokana na utepetevu wa madaktari katika Hospitali ya Wesu, Taita Taveta.

Kulingana na ripoti, mtoto Mwasi alizaliwa mnamo Januari 21, 2024, saa tisa kasoro dakika 10 katika Hospitali ya Wesu akiwa na uzani wa gramu 3,300.

Ripoti hiyo iliwasilishwa mbele ya Seneti kujibu swali lililoulizwa na Seneta Maalum Hamida Kibwana.

Hata hivyo, mnamo Januari 29, 2024, siku nane tu baada ya kukaribishwa duniani, madaktari katika Hospitali Kuu ya Pwani–Coast General–waliafikiana kumkata mtoto huyo mkono uliokuwa umepooza kabisa licha ya kutibiwa katika Hospitali ya Wesu na Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi.

Yote yalianza wakati mama yake mtoto Mwasi aligunduliwa kuwa na matatizo kwenye mfuko wa uzazi alipokuwa akijifungua, Seneti ilielezwa.

“Wakati wa kujifungua, mama aligunduliwa kuwa na matatizo. Kwa kushuku huenda mtoto alikuwa ameathirika, mchakato wa kumtibu ulianzishwa ambapo tabibu aliyekuwa kwenye zamu alipendekeza sindano. Hii ilihitaji dawa kupitishiwa mshipa, shughuli iliyofanikishwa kupitia mkono wa kulia,” ilisema ripoti iliyowasilishwa na Wizara ya Afya ya Kaunti ya Taita Taveta.

Mnamo Januari 23, 2024, saa 36 baadaye, muuguzi aliyekuwa kwenye zamu aligundua kifaa cha kuzuia mzunguko wa damu kikiwa kingali kimefungwa kwenye sehemu ya juu ya mkono wa kulia wa mtoto.

Baada ya ukaguzi, ilibainika mkono ulikuwa umefura na kudhoofika. Afisa wa Matibabu siku hiyo aliwasiliana na mwenzake katika Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi na kushauriwa kuendelea kumpa mtoto matibabu na kumfanyia ukaguzi wa CT Scan.

“Januari 24, Afisa wa Matibabu alishauriana na mtaalam wa upasuaji na akaagizwa afanye uchunguzi wa CT lakini mashine ya haikuwa ikifanya kazi. Januari 25, mkono ulionyesha dalili za kupata nafuu lakini vidole vilikuwa bado vimepooza. Uamuzi ulifanywa kuendelea na matibabu,” ripoti ikaeleza.

Seneti ilisikia kuwa mnamo Januari 29, 2024, mkono haukuonyesha dalili zozote za kupona ambapo uamuzi ulifanywa kumpeleka katika Hospitali ya Voi kwa matibabu zaidi, kabla ya kuhamishwa siku hiyo hiyo jioni katika Hospitali Kuu ya Pwani

“Kutokana na ukosefu wa Mashine ya CT Scan katika hospitali ya Moi Voi wakati huo, mtoto alihamishwa katika Hospitali Kuu ya Pwani. Uamuzi ulifanywa kukata mkono huo katika sehemu ya juu ya kiwiko.”

Kufuatia tukio hilo lililoibua hasira, Waziri wa Afya Kaunti ya Taita Taveta ameandikia Baraza la Maafisa wa Kliniki kuanzisha uchunguzi huku maafisa waliomhudumia Mtoto Mwasi katika kipindi hicho akiwemo Afisa aliyekuwa kwenye zamu, wakisimamishwa kazi.

“Imedaiwa kuwa, akiwa kwenye zamu Januari 21,2024, katika Hospitali ya Wesu, Taita Taveta, Afisa wa Kliniki aliyesajiliwa aliyetajwa hapa alitelekeza wajibu wake na kusababisha mtoto mchanga kupooza na kisha kukatwa mkono wake wa kulia,” aliandika Bw Gifton Mkaya.