Madhara ya kuongezea chumvi kwenye chakula
NA WANGU KANURI
KUONGEZEA chumvi kwenye chakula chako kunakuweka kwenye hatari ya kansa ya tumbo kwa asilimia 40 – utafiti umeonyesha.
Wanasayansi wanashauri kuwa hupaswi kutumia zaidi ya kijiko kimoja kidogo cha chumvi kwenye chakula chako.
Hii ni kwa sababu viungo vingi vinavyotumika kupika huwa na chumvi na unapoongezea, inakuwa na madhara. Zaidi ya kansa ya tumbo, anayetumia chumvi nyingi yupo kwenye hatari ya magonjwa kama shinikizo la damu, mshtuko wa moyo na kiharusi.
Hata hivyo, utajua iwapo umetumia chumvi nyingi iwapo unapata maumivu ya kichwa baada ya kula.
Hii ni kwa sababu chumvi nyingi humfanya mtu akose maji ya kutosha mwilini na akapata maumivu haya ya kichwa baada ya saa moja au mbili.
Pili, iwapo miguu na mikono yako inafura. Baada ya kula chumvi nyingi, figo hufanya mwili kuondoa maji kidogo kwenye mwili hivi kusababisha ongezeko la ugonjwa wa shinikizo la damu.
Pia, baada ya kula chumvi nyingi dalili kama kutoona vizuri, maumivu kwenye kifua, kuhisi kama hupumui vizuri na kutokwa na damu kwenye pua (nosebleed) humfanya mtu kupata ugonjwa wa shinikizo la damu.
Mwishowe, kula chumvi nyingi hufanya mtu kuenda haja ndogo sana. Hali hii husababishwa na mwili kuhisi kiu kingi ili kuondoa chumvi hiyo iliyojaa mwilini.