Habari za Kaunti

Pangani Lamu: Wanawake ndio kusema katika biashara ya maziwa

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

UKIWAPATA akina mama wakikusanyika kando ya barabara asubuhi na mapema, huku wakiwa wameshikilia vibuyu mikononi, utadhani wanataka kuenda kuteka maji ziwani au wakisubiri kuabiri gari au pikipiki kuelekea mahali fulani.

Taswira hiyo, ambayo imedumu kwa miaka mingi, sasa imegeuka kuwa kitambulisho kamili kwa wale wasiokijua vizuri kijiji cha Pangani kilichoko Lamu Magharibi.

Kijiji hicho kinapatikana kati ya Kibaoni na Witu.

Ni makazi ya wafugaji, hasa jamii ya Wasomali.

Pangani ni kijiji kinachovuma ndani na nje ya Lamu kwa biashara ya maziwa, ambapo wanawake hapa ndio kusema.

Akina mama ndio huinogesha biashara hiyo kila siku, iwe ni asubuhi na mapema au nyakati za jioni kabisa.

Kijiji cha Pangani kiko katikati ya barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, ambapo barabara hiyo hukipasua katikati, hivyo kukigawanya pande mbili.

Ni kijiji ambacho kimekuwepo tangu miaka ya sabini (1970s), ambapo kwa wakati huo kilikuwa kikitumiwa kama makazi ya muda ya jamii za wafugaji wa kuhamahama ambao walikuwa wakitoroka makazi yao ya Ijara, Kaunti ya Tana River na kukimbilia Pangani kila wakati ukame unapoathiri maeneo yao.

Ni eneo hilo la Pangani ambapo wafugaji walifaulu kujipatia malisho na maji kwa mifugo wao, hivyo kuishi raha mustarehe.

Sehemu mojawapo ya kijiji cha Pangani, Lamu kinachovuma kwa biashara ya maziwa inayoendeshwa na akina mama. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wafugaji hao wa kuhamahama hata hivyo walianza kujenga makazi ya kudumu Pangani kati ya mwaka 2005 na 2007, hivyo kufanya eneo hilo kuwa kijiji kamili cha wafugaji.

Taifa Leo iliazimia kujua kwa nini akina mama hapa Pangani ndio kusema katika biashara ya maziwa?

Kulingana na Msemaji wa Wafugaji, Kaunti ya Lamu na mzee wa Kisomali, Bw Muhumed Kalmei, ni kawaida kwa wanawake, hasa wale wa jamii ya Wasomali kujitosa mazima katika shughuli za kuuza maziwa.

Aliitaja mila ya Wasomali kwamba humtambua sana mwanamke kuwa mwenye kuwajibikia suala la kukama ng’ombe na kutayarisha maziwa na hata kuyapeleka sokoni.

“Hawa wanawake wengi unaowaona Pangani wakiuza maziwa barabarani wanadhihirisha wazi mila yetu ya Kisomali. Sisi Wasomali tunatambua kabisa kuwa mwanamke ndiye anayepaswa kukama ng’ombe, kutayarisha maziwa na kuyauza sokoni. Wanaume hujishughulisha sana na kazi nyingine, ikiwemo kupeleka ng’ombe na mifugo mingine malishoni,” akasema Bw Kalmei.

Ni kwenye kijiji cha Pangani ambapo mara nyingi utapata magari aina ya probox yaliyofungwafungwa vibuyu upande wa juu na hata ubavuni yakiwa yameegeshwa kando ya barabara huku wenye magari hayo wakinunua maziwa kutoka kwa akina mama na kuyasafirisha hadi katika maeneo mengine ya Lamu na kaunti nyingine za Kenya.

Gari aina ya probox likiwa limeegeshwa kando ya barabara ya Lamu-Witu-Garsen katika eneo la Pangani ambapo kusudio ni mwenyewe kununua maziwa kutoka kwa wakazi, wengi wakiwa ni wanawake. Wanawake kijijini Pangani ndio kusema katika biashara ya maziwa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hapa, maziwa katika kibuyu cha lita tano (5) huuzwa kwa kati ya Sh300 na Sh400.

Bi Halima Abdulrahman, mmoja wa wauzaji mashuhuri wa maziwa kijijini Pangani, anasema bei ya bidhaa hiyo hubadilikabadilika kulingana na msimu.

Bi Abdulrahman anaeleza kuwa msimu wa kiangazi au ukame hufanya bei ya maziwa kupanda ilhali wakati wa masika, bei hushuka.

“Utapata kibuyu cha lita 5 kikiuzwa kati ya Sh300 na Sh400 msimu wa masika ilhali kiangazi au ukame unapoanza, bei hupanda hadi kati ya Sh400 na Sh600 kwa kibuyu hicho hicho cha lita 5. Wakati wa ukame maziwa hutoka kidogo au kupungua kwani nyasi za kulisha mifugo wetu huwa hakuna,” akasema Bi Abdulrahman.

Bi Khadija Yusuf, muuzaji mwingine wa maziwa Pangani, aliisifu biashara hiyo, akiitaja kuwasaidia kusomesha watoto wao.

Bi Yusuf ni mama wa watoto sita.

Anasema alianza kuuza maziwa karibu miaka kumi iliyopita.

“Utashangaa kwa nini ni akina mama tu wanaouza maziwa Pangani. Sisi ndio hurauka kukama ng’ombe na kuleta maziwa hapa barabarani mapema. Hilo huwapa fursa waume wetu kufungua ng’ombve kwenda malishoni. Twasaidiana kimajukumu. Biashara ya maziwa ni nzuri. Mimi binafsi imenisaidia kusomesha wanangu watatu sekondari,” akasema Bi Yusuf.

Mbali na maziwa yanayouzwa yakiwa mabichi, akina mama wa Pangani pia wamejitahidi kuyagandisha maziwa, kuyachuja na kuyatengeneza samli na kisha kuiuza barabarani.

Kuna wengine ambao pia wamekuwa wakitumia maziwa hayo hayo kutengeneza labania na kisha kusafiri mjini Witu kuiuza.

Ni kutokana na umaarufu wa Pangani katika kuendeleza biashara ya maziwa ambapo kijiji hicho siku za hivi karibuni kimepandishwa hadhi na kuwa kituo maalumu cha kukusanyia maziwa na kuyauza kwa jumla kwa madalali na wapitanjia.

Hapa, utapata wafugaji wa vijiji jirani kama vile Lumshi na Widho wakisafiri kufika Pangani kupeleka au kuwasilisha mitungi yao ya maziwa kuyauza.

Baadhi ya wakazi wa Pangani na viunga vyake waliohojiwa na Taifa Leo waliomba serikali ya kaunti, ile ya kitaifa na wadau mbalimbali kufikiria kuwajengea kiwanda cha maziwa eneo hilo ili kuifaidi zaidi kutokana na bidhaa hiyo.

“Ng’ombe ni wengi hapa Pangani. Wauzaji maziwa kutoka Pangani, Lumshi na Widho pia wamekuwa wakikutana hapa kwa wingi kuuza maziwa kwa wapita njia au madalali. Itakuwa bora tukianzishiwa kiwanda cha maziwa hapa ili tuifaidi zaidi hii biashara yetu ya maziwa. Najua kuwepo kwa kiwanda kama hicho kutatuletea soko la karibu na la uhakika hapa Pangani,” akasema Bi Fatma Wako.