Siasa

Joho aahidi kuvumisha ODM kila kona ya nchi

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WINNIE ATIENO

NAIBU Mwenyekiti wa Orange Democratic Movement (ODM), Bw Hassan Joho, ameapa kukiuza chama hicho cha upinzani kila kona ya nchi ili wapate uungwaji mkubwa na wafuasi kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Joho ambaye amekita kambi eneo la Nyanza kusaka wafuasi, alisema atahakikisha vyama vingine havipenyi eneo hilo ambalo limekuwa ngome ya kinara wa ODM Bw Raila Odinga.

Alisema kampeni mpya ya ODM huko Nyanza pia inanua kuhakikisha umoja wa wanachama wa upinzani.

Akiongea na wanachama huko Nyatike, Bw Joho alisema atazuru nchi nzima kusaka uungwaji mkono akisisitiza kuwa chama cha ODM kitaunda serikali.

“Nitavyoga kila kona ya hii Kenya kuuza chama changu na mipango ya siku za usoni ya kuunda serikali ya ODM mwaka wa 2027,” alisema Bw Joho ambaye aliandamana na aliyekuwa mpinzani wake wa kisiasa Bw Suleiman Shahbal ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Bw Shahbal alimteja Bw Joho kuwa ni mwanasiasa shupavu ambaye amekuwa akitetea rasilimali za wapwani ikiwemo bandari ya Mombasa.

“Siku moja, Bw Joho alisimama mbele ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kumwambia kuwa hawezi kuchukua bandari yetu ya Mombasa. Mtu anayetaka Urais lazima awe na nguvu, moyo wa ushujaa na asiyeogopa mtu,” alisema Bw Shahbal.

Alisema Bw Joho ni kiongozi shupavu asiyeogopa yeyote.

Bw Shahbal alieleza namna aling’ang’ana na Bw Joho kwenye safari yake ya kisiasa wakawa mahasimu wakubwa na hatimaye marafiki.