Familia yatafuta Sh200,000 kurudisha mtoto aliyekwama Misri
NA GITONGA MARETE
FAMILIA moja kutoka Kaunti ya Meru inaomba msaada wa zaidi ya Sh200,000 ili kumrejesha mwana wao ambaye ni mgonjwa na anaendelea kuzuiliwa nchini Misri baada ya muda wa pasipoti yake inayomruhusu kuishi huko kupitwa na wakati.
Familia ya Linet Makena ambaye amejaaliwa mtoto anayeugua anemia (upungufu wa damu mwilini) imesema kuwa alikuwa akifanya kazi kama mjakazi lakini akaishia kuwa gerezani baada ya cheti hicho kupitwa na wakati.
Bi Makena anauzuiliwa baada ya serikali ya Misri kuendesha oparesheni dhidi ya wahamiaji haramu na wakati huo hakuwa amerefusha muda wa kutumia pasipoti yake kutokana na ukosefu wa hela.
Amekuwa akifanya kazi Misri tangu 2018 na alijaaliwa mtoto mnamo Disemba 4, 2019 kutokana na uhusiano ambao alikuwa nao na raia wa Tanzania aliyekuwa pia akifanya kazi huko. Hata hivyo, mwanaume huyo amemtelekeza na hata alisharejea kwao huku akimwacha Bi Makena na kazi kubwa ya kumlea mtoto huyo.
Hali hiyo imefanya mamake Julia Mwitari asononeke huku akisikitishwa na habari zaidi kuwa mwanawe na mjukuu wake wote wanaugua na wanapitia changamoto tele za maisha. Mjukuu wake kwa sasa anaishi na rafikiye Bi Makena huku Misri.
Japo familia ilianzisha juhudi za kuchangisha pesa zinazohitajika, ugumu wa uchumi umedhihirika huku Sh2,000 pekee zikitolewa na marafikize aliowajumuisha katika ukumbi wa WhatsApp.
Bi Mwitari ambaye anaishi jijini Nairobi alisimulia kuwa kabla ya madhila hayo yatokee, Bi Makena alikuwa akituma hela nyumbani na kumsaidia kukimu maisha yake.
“Siku ambayo alikamatwa, tulizungumza kupitia mtandao wa Skype na akaniambia yeye ni mgonjwa na hana pesa za kuenda kupokea matibabu hospitalini. Nilimwaambia kuwa ningekuwa na kipande cha ardhi, ningekiuza ili tupate pesa za kumrejesha nyumbani. Baadaye siku hiyo jioni nilipata habari kuwa alikuwa amekamatwa kama mhamiaji haramu,” Bi Mwitari akaambia Taifa Leo.
Nyumbani kwao Ruiri, Kaunti Ndogo ya Buuri, familia yao imejawa na huzuni huku shangazi yake akisikitika kuwa alizungumza mara ya mwisho na Bi Makena Machi mwaka huu.
Mjombake John Muthuyia naye aliwaomba viongozi wa Kaunti ya Meru wawasaidie kumrejesha Bi Makena nyumbani.
“Tunaambiwa hali vizuri chakula na kama wakulima itatuchukua muda mrefu sana kupata pesa zinazohitajika. Tunawaomba viongozi na wahisani watusaidie kumrejesha Makena nyumbani,” akasema Bw Muthuyia.