Habari za Kaunti

Shirika lasaidia wasichana 10,000 Kibra kupata taulo za hedhi

May 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

ZAIDI ya wasichana 10,000 wamenufaika kwa kupata taulo za hedhi kwa miaka mitatu sasa kupitia mpango ambao umekuwa ukiendeshwa na Shirika la Christian Best Camp mtaani Kibra.

Shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kufanikisha elimu ya mtoto wa kike pamoja na kutekeleza miradi ya kuinua maisha ya wakazi katika mtaa huo wa mabanda ambao una viwango vya juu vya umaskini.

Mnamo Jumanne, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani, Christian Best Camp ilitangaza kuwa imeanzisha kituo kikuu mtaani Kibra.

Wakenya wako huru kufika kituo hicho kisha kuchangia taulo zao za hedhi kwa wasichana ambao hawajabahatika katika jamii. Pia shirika lenyewe litakuwa likitoa taulo hizo katika ziara mbalimbali kwenye shule za mtaa huo.

“Ni jambo la kuaibisha kuwa wasichana bado enzi hizi hawawezi kufika shuleni wakati ambapo wanapitia hedhi. Hiyo ndiyo sababu tulianzisha kituo ambacho wahisani hufika kisha kutoa taulo za hedhi kuwasaidia wanafunzi wa kike wanaoishi kwenye mitaa hiyo,” ikasema taarifa kutoka Christian Best Camp.

Baadhi ya wasichana walionufaika na mpango wa utoaji taulo za hedhi katika kituo cha CBCK mnamo Mei 28, 2024. PICHA | CECIL ODONGO

Shirika hilo lilishukuru kwa ushirikiano ambao umekuwepo kati yao na jamii na viongozi wa kisiasa ambao umesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya kuwainua watoto wa kike.

“Tunalenga kuongeza idadi ya wasichana ambao hunufaika na kuendelea kuhakikisha kuwa suala la hedhi si kikwazo tena kwa elimu ya mtoto wa kike hasa katika mitaa ya mabanda,” ikaongeza taarifa hiyo.