Habari za Kaunti

Bunge la Kisii: Mnara wa aibu?

May 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WYCLIFFE NYABERI

KIZAAZAA kilishuhudiwa katika Bunge la Kaunti ya Kisii mnamo Jumanne, madiwani wa kaunti hiyo waliporushiana cheche za maneno na hata kutishia kulimana makonde.

Vimbwanga hivyo vilijiri kufuatia tofauti zilizozuka baina yao walipokuwa wakijadili hoja ya kumng’atua kazini Waziri wa Maswala ya Utawala wa Kaunti ya Kisii Dkt Alfred Ndemo.

Hata hivyo, hoja hiyo haikufaulu kwani madiwani 43 walipiga kura ya kumwokoa Dkt Ndemo. Ni madiwani 24 pekee waliotaka amwage unga.

Kizaazaa kilianza wakati diwani wa Bokimonge Amos Onderi, aliomba kura ya kuamua mustakabali wa Dkt Ndemo ipigwe bila kufuata utaratibu wa kuyaita majina ya madiwani kama yanavyofuatana kialfabeti.

Bw Onderi alidai kwamba ikiwa mtiririko wa alfabeti ungefuatwa, ingekuwa rahisi kwa watu fulani katika serikali ya Kisii–ambao hakuwataja–kujua jinsi walivyopiga kura zao na hivyo hilo lingewazuia kufanya maamuzi yao kwa busara inayotakikana.

Baada ya kurushiana cheche za matusi na kunyoosheana kidole cha lawama, Spika wa kikao hicho cha alasiri Bw Jacob Bagaka, aliamuru madiwani wapige kura jinsi ambavyo majina yao yanavyotiririka kialfabeti.

Hii ni mara ya pili kwa waheshimiwa hao kuvutana mashati mwaka huu 2024.

Mnamo Februari, madiwani hao walitishia kunyanyuana wakati walikuwa wakijadili hoja ya kumng’atua afisini aliyekuwa naibu gavana wa jimbo hilo Dkt Robert Monda.

Hoja ya kumng’atua kazini Dkt Ndemo iliwasilishwa bungeni na diwani wa Bogeka Richmond Manani akimshtumu kwa matumizi mabaya ya afisi yake, miongoni mwa sababu nyingine.

Diwani maalum Dolphine Bwari wa UDA aonyesha hasira zake wakati wa kujadiliwa hoja ya kumtimua afisini Waziri wa Maswala ya Utawala wa Kisii Dkt Alfred Ndemo. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Kabla ya kujadiliwa kwa hoja ya Dkt Ndemo, baadhi ya madiwani walisikika wakisema ikiwa hakuna pesa, basi hoja hiyo ingeanguka.

“Ikiwa hakuna pesa, hakuna kumng’atua afisini Dkt Ndemo,” diwani mmoja alisikika akisema bungeni kwa makeke.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kuanza kumuunga mkono Gavana wa Kisii Simba Arati, Dkt Ndemo alikuwa mwaniaji mwenza wa Bw Manson Oyongo, aliyekuwa alishindana na Bw Arati kwenye wadhfa huo katika uchaguzi wa Agosti 2022.

Katika tukio la kustaajabisha, Dkt Ndemo ‘alimruka’ Bw Oyongo dakika za mwisho na kutangaza kwamba alikuwa amejiunga na Bw Arati.

Baada ya kumpa kazi ya uwaziri, gavana Arati alishangaza wengi baada ya muda fulani alipomtuma Dkt Ndemo kwa likizo ya lazima kwa sababu zisizoeleweka.

Ili kulalamikia uamuzi huo, Dkt Ndemo alielekea mahakamani na kushinda kesi ya hujuma dhidi yake.

Hoja iliyolenga kumng’atua afisini Dkt Ndemo iliwasilishwa bungeni baada ya mahakama kumpa afueni ya kumrejesha kazini.

Akizungumza na wanahabari baada ya hoja hiyo kufeli, diwani wa Marani Bw Dennis Ombachi alisema walifanya uamuzi wao kwa njia huru bila kushurutishwa na mtu yeyote.

“Hatuwezi kukubali kutumika kisiasa na kuwaharibia watu wetu majina kwa kuwang’atua. Dkt Ndemo ni msomi na hakuna makosa yoyote tuliyoona kwenye hoja dhidi yake. Tunamwambia gavana Arati ashirikiane na mawaziri wake kuwahudumia wakazi wa Kisii. Tuache drama,” Bw Ombachi alisema.