Makala

Mbunge asimulia jinsi alivyolazwa kwa mtaro kuepuka kifo

May 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Thika Mjini Bi Alice Ng’ang’a mnamo Jumatano alisimulia jinsi alivyoponyoka mauti alipotupwa kwa mtaro wa majitaka na maafisa wa usalama waliomuokoa wakati ghasia zilichipuka katika eneo la Kiganjo mnamo Mei 17, 2024.

Bi Ng’ang’a alisema kuna watu mashuhuri ambao wanataka kumwangamiza kwa kuwa wanamuonea wivu kwa jinsi anavyochapia watu wake wa Thika Mjini kazi na hatimaye kuwarai wampandishe ngazi kama njia ya shukran hadi awe gavana mwaka 2027.

Ghasia hizo ambazo zilisababisha kifo cha kijana mmoja baada ya kupigwa risasi, zilizuka wakati Bi Ng’ang’a alifika katika uwanja unaopenedekezwa kujengwa soko la Kiganjo lakini kukawa na makabiliano ya magenge. Ni hali ambayo ilimwangazia mbunge wa Gatundu Kusini Bw Gabriel Kagombe akifyatua risasi kiholela akilenga raia.

Baadaye Bw Kagombe alichapisha picha mtandaoni akiwa hospitalini kwa kile alidai ni kutibiwa majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa.

Wabunge wengine ambao walikuwa katika kizazaa hicho lakini wakakwepa mambo yalipochacha ni pamoja na wa Kikuyu Bw Kimani Ichung’wa na ambaye ndiye Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa, mbunge wa Juja Bw George Koimburi na mwenzao wa Gatundu Kaskazini Bw Elijah Kururia.

Bw Kagombe aliishia kujiwasilisha hadi hospitali moja ya kibinafsi alikolazwa kwa madai kwamba hata yeye aliumizwa katika patashika hizo.

Sasa, Bi Ng’ang’a akiongea katika runinga ya Inooro, alisema lengo kuu la uvamizi huo lilikuwa kumwangamiza na wasingekuwa ni maafisa wa usalama kufanya hima na wakamlaza kwa mtaro ili kumkinga asipatwe na risasi pamoja na vifaa vingine butu vilivyokuwa vikirushwa, kwa sasa angekuwa ashaenda zake kuzimu.

“Niliona mauti kwa haya macho yangu mawili… Nilikuwa nimefika katika uwanja huo kukabidhi kwa mwanakandarasi mradi wa ujenzi wa soko kwa kima cha Sh54 milioni, mradi ambao unafadhiliwa na serikali kuu. Lakini nilikumbana na magenge ambayo yalinilaki kwa mawe na kila aina ya silaha na matusi na katika mshikemshike uliozuka, ikawa hali si hali tena nikipambana kuhifadhi uhai wangu,” akasema Bi Ng’ang’a.

Bi Ng’ang’a aliongeza kwamba maafisa wa usalama waliokuwa wamemkinga asiuawe walipata majeraha.

“Mmoja aligongwa kwa mawe usoni, mwingine akagongwa jiwe kifuani kushoto huku naye kijana aliyekuwa akinikinga akikatwa kwa upanga kwa kichwa,” akasema.

Bi Ng’ang’a alisema kwamba aliondoka mahali hapo baada ya maafisa wa polisi kuthibiti hali kupitia kurusha vitoa machozi na kufyatua risasi juu angani “na ndipo nilitoroshwa kupitia gari jingine kwa kuwa langu lilikuwa limepigwa vioo kwa mawe”.

“Niliondoka eneo hilo nguo zangu zikiwa na damu ya waathiriwa wa ghasia hizo na pia nikiwa nimepoteza viatu vyangu,” akasema.

Alisema kwamba yuko na majonzi tele kufuatia kifo cha David Nduati,26, kijana aliyeaga dunia akimpigania asiumizwe na magenge hayo yaliyokuwa yamesafirishwa hadi Kiganjo na wale alidai ni mahasidi wake.

“Ningetaka idara husika za kudumisha usalama zitie bidii na kuwakamata wale wote ambao walihusika na ghasia hizo na kisha kusababisha kifo. Hata ikiwa mimi ndiye nitapatikana kwa lawama, nafaa nishikwe. Hizo zilikuwa ghasia za kisiasa zikilenga kunizima kuwapa watu wa Kiganjo mradi wa soko ambalo mimi ndiye nimelisaka kutoka kwa serikali kuu na pia nikatafuta ardhi ya wapi mradi huo ujengwe,” akasema.

Bi Ng’ang’a alisema kwamba kwa sasa ametafuta miradi mitano ya masoko ambayo yatajengwa katika maeneo ya Kiganjo, Ngoingwa, Madaraka, Maguguni na Kiandutu “na pia nikilenga kusaka mengine zaidi ya 20 kabla ya awamu yangu ya ubunge kutamatika 2027”.

Alisema kwamba nia yake siku hiyo haikuwa vita “na ndio sababu hata sikuwa nimejihami kwa bunduki yangu wala kuandamana na walinzi wa kujihami”.

Aliwataka wale wanaomuona kuwa tishio katika siasa zao waelewe kwamba “mimi nimetangaza kuwa nalenga kuwa gavana 2027 na hivyo basi wawe wakinitumia magenge ambayo yako na magavana ndani yake badala ya hawa wanatumwa wakiandamana na madiwani”.