Kocha Vincent Kompany apata kazi Bayern licha ya Burnley kuteremka
NA MWANGI MUIRURI
LICHA ya kocha Vincent Kompany kutofaulu kuisaidia Burnley kusalia katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), safu ya kandanda imemtuza majukumu ya kuinoa timu ya Bayern Munich inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani almaarufu Bundesliga.
Ingawa Kompany ndiye alikuwa ameiongoza Burnley kupandishwa ngazi hadi EPL kutoka ligi ya daraja la pili Uingereza katika msimu wa 2022-24, alipotua EPL alijipata akigeuka kuwa vibonde na akamaliza ligi hiyo katika nafasi ya 19 kati ya zote 20.
Kati ya mechi zote 38 alizosimamia Burnley katika msimu wa EPL wa 2023-24, Kompany alishinda mara tano pekee, akatoka sare mara tisa na akapoteza mara 24.
Katika safari hiyo ya kupigwa, timu yake ilitikisa nyavu za wapinzani mara 41 nayo ikitikisiwa zake mara 78 hivyo basi ikimaliza kwa ubora wa mabao -37. Hii ni kumaanisha kulikuwa na nakisi.
Kompany alishinda timu ya Shefield United na kwa pamoja na Luton Town iliyokamata nafasi ya 18 katika jedwali, wakapigwa shoka kutoka EPL.
Sasa Kompany, ambaye ana umri wa miaka 38 amedhihirisha kuwa mpira hauna adabu wala heshima kwa mtazamo ule ulio na wengi na ambao ni kwamba waliofuatilia visanga vya Burnley kwa sasa wanamuona kama aliyefeli katika majukumu yake.
Hata hivyo, Kompany ambaye ni raia wa Ubelgiji ameonekana na wadau wa soka Ujerumani kuwa ‘mchawi’ wa soka ambaye ataifanikisha timu hiyo ya Bayern Munich iliyomaliza msimu wake wa 2023-24 ikiwa ya tatu katika ligi hiyo ya Bundesliga.
Ilijizolea pointi 72—matokeo yake duni zaidi tangu 2010/11—nyuma ya Bayer Lerverkusen iliyopata pointi 94 bila kupoteza mechi yoyote kati ya zote 34 na kutawazwa mabingwa, na pia timu ya VfB Stuttgart iliyolala kwa pointi 73 ikiwa ya pili.
Kompany sasa atarithi mikoba ya kocha Thomas Tuchel na tayari ametoa taarifa akishukuru kwa kuaminiwa katika majukumu hayo mapya.
“Bayern Munich ni taasisi katika ulimwengu wa soka,” akasema kwa kusifia.
Kompany ambaye ni difenda wa zamani wa timu ya Manchester City na aliyeangika daluga mwaka wa 2020, amepewa kandarasi ya miaka mitatu ndani ya Munich.
Kompany aliangukia majukumu hayo ya Bayern Munich baada ya makocha Xabi Alonso wa Lerverkusen, mwenzake wa timu ya taifa ya Ujerumani Julian Nagelsman, kocha wa taifa la Austria Ralf Rangnick pamoja na Tuchel kuyakataa.
Mkurugenzi wa Masuala ya Spoti wa Bayern Munich Christoph Freund amenukuliwa akisema kwamba “Kompany ni kocha ambaye anawiana na utamaduni, itikadi na nembo za timu hii yetu”.