Mwanamke aliyeshtakiwa kulaghai Sh25m kwa mwekezaji aachiliwa kwa dhamana
NA RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA ya Milimani imemwachilia kwa dhamana ya Sh5 milioni mfanyabiashara anayetumia jina la kinara wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga kuwalaghai wawekezaji.
Hakimu mkazi Ben Mark Ekhubi alimwachilia Faith Mwikali Ndiwa anayeshtakiwa kumlaghai mwekezaji kutoka Nigeria, Jude Olabayo Veracruz Sh25 milioni baada ya kukaa rumande siku nne.
Akimwachilia kwa dhamana, Bw Ekhubi alisema upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha korti kumnyima dhamana Mwikali.
“Ushahidi kwamba mshtakiwa amepokea pesa nyingi kutoka kwa wawekezaji kwa njia ya ulaghai na kwamba atazitumia kutoroka sio sababu tosha kuwezesha mahakama kumnyima dhamana,” alisema hakimu.
Hakimu huyo alisema ni haki ya mshtakiwa kuwa na pasipoti na kusafiri kwake ng’ambo mara nyingi sio sababu tosha kuwezesha mahakama kumnyima dhamana.
“Sio hatia kwa Mkenya kumiliki cheti cha usafiri. Ni haki ya kila Mkenya kumiliki pasipoti,” alisema Bw Ekhubi.
Mbali na kuweka dhamana ya Sh5 milioni au dhamana ya pesa taslimu Sh1 milioni, hakimu alimtaka mshtakiwa awalete watumishi wawili wa umma kumthamini kabla ya kuachiliwa kutoka gerezani.
Mahakama vilevile ilimwamuru mshtakiwa awe akifika mbele ya afisa anayechunguza kesi hiyo mara mbili kwa mwezi.
Bw Ekhubi pia aliagiza mshtakiwa awasilishe cheti chake cha usafiri kortini.
Mwikali alifikishwa kortini Jumatatu wiki hii na kukana shtaka la kumlaghai Veracruz Sh25 milioni akidai alikuwa ameshinda zabuni ya kuuzia mamlaka ya usambazaji dawa (Kemsa) neti zilizotibiwa kuzuia watu kuumwa na mbu.
Punde tu baada ya kuagiza mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana mawakili Nicholas Kamwendwa, Danstan Omari na Kibet Cheboi waliomba mahakama iamuru mshtakiwa apelekwe hospitali kwa vile alikumbwa na changamoto ya kiafya akiwa rumande.
Hakimu aliamuru mshtakiwa apelekwe hospitali kabla ya kutia sahihi cheti cha kuachiliwa kutoka rumande.
Mwikali alikana mashtaka nane ya ulaghai na upokeaji pesa kwa njia ya udanganyifu.
Akimshawishi Veracruz ampe pesa hizo mshtakiwa anadaiwa alimweleza kwamba zabuni hiyo ya kuuzaji Kemsa neti zilizotibiwa za kujikinga na mbu ilikuwa imepewa mkwewe Bw Odinga na kwamba ameshindwa kuikamilisha kutokana na uhaba wa fedha.
Veracruz alielezwa atapewa kitita kizuri cha pesa neti hizo zikiuziwa Kemsa.
Pia hakimu alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Virginia Kariuki kwamba mshtakiwa anayetumia majina mengine- Eunice Karehu, Faith Nthiwa na Faith Mwikali Ndiwa amemlaghai muwekezaji mwingine Samson Kikaya Sh27 milioni.
Bw Ekhubi alielezwa na afisa anayechunguza kesi hiyo Kipario Lekakeny kwamba mshtakiwa pia hujitambua kama Daktari wa kibinafsi Raila Odinga na Meneja wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Maendeleo (UNDP).
Bw Lekakeny alikuwa amepinga ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana akisema “kuna uwezekano mkubwa mshtakiwa atatoroka akitumia majina feki.”
Bi Kariuki aliomba mahakama ikawie kumwachilia Mwikali kwa dhamana hadi polisi wabaini jina lake kamili.
Kamwendwa, Omari na Kibet Cheboi walipinga ombi la serikali wakisema “hakuna sababu zilizo na mashiko kisheria yanayoweza zuia mahakama kumwachilia kwa dhamana.”
Hakimu aliamuru kesi dhidi ya mshtakiwa litajwe Juni 21 kwa maagizo zaidi.