Habari za Kaunti

Mbunge asisitiza vita dhidi ya muguka vingalipo

May 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MAUREEN ONGALA

MBUNGE wa Ganze Bw Kenneth Kazungu amesisitiza kwamba vita dhidi ya muguka vitaendelea bila uoga wowote katika Kaunti ya Kilifi.

Akihutubu katika Shule ya Msingi ya Bale wakati wa kuzindua rasmi ukarabati wa madarasa mabovu, Bw Kazungu alisema ni wajibu wa Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhakikisha vijana waraibu wa muguka wanaachana na bidhaa hiyo.

Bw Kazungu alisema kuwa hata baada ya mkutano na viongozi kutoka Kaunti ya Embu wakiongozwa na gavana Cecily Mbarire, Rais Ruto hakuwahusha viongozi wa Pwani kabla ya kutoa taarifa ya Ikuku kuhusu muguka.

“Tunapoteza kizazi chetu na ndio maana tunapinga muguka. Rais alichukua hatu bila kuhusisha viongozi wa Pwani na cha kushangaza ni kuwa alitenga Sh500 milioni za uongezaji thamani kwa mmea wa muguka,” akasema Bw Kazungu.

Aliwataka viongozi hao wakuu serikalini wasikize sauti za viongozi wa ukanda wa Pwani ambao wamesiama kidete kupigania jamii ambayo inaangamia kufuatia uraibu mkubwa wa muguka.

Wakati mbunge huyo akitoa kauli hiyo, wakazi wa Kaunti ya Kilifi  walifanya maandamano mnamo Alhamisi kupinga biashara ya muguka wakidai ina athari mbaya kwa vijana, wanawake na watoto.

Maandamano ya kupinga muguka Kilifi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Mbunge huyo wa Kenya Kwanza alisema kuwa inashangaza kuwa naibu rais amelifumbia macho swala la muguka wakati alikuwa mstari wa mbele kupiga vita mihadarati na pombe haramu.

Aliwataka madiwani katika mabunge ya kaunti za Kilifi, Mombasa na Taita-Taveta kuongeza ushuru wa muguka katika sheria mpya za uchumi.

“Ninapendekeza bei ya chini ya muguka iwe Sh1,000 ili kuwazuia watoto wetu kununua bidhaa hiyo,” akasema.

Bw Kazungu alisema kuwa viongozi wa pwani watawasilisha mswada bungeni kurekebisha sheria na kutoa miraa na muguka kuwa ni miongoni mwa mimea ya mavuno inayotambuliwa nchini.

Alisema vita dhidi ya muguka vinaungwa mkono na viongozi wote wa Pwani, Kaskazini Mashariki na pia wale wa kutoka Magharabi mwa nchi.

Alikosoa agizo la Mahaka Kuu ya Embu kwa kukosa kumlinda mpwani kutokana na mmea huo aliodai ni hatari.

Mwenyekiti wa kundi la kina mama la kutetea haki za wanawake na watoto Bi Kibibi Ali alisema kuwa kwa sasa athari za muguka zimesambaa Pwani nzima.

Mwaka 2018 aliongoza akina mama kupinga muguka japo hakuna hatua mwafaka iliyochukuliwa na viongozi husika.

“Tuliandamana kupinga muguka katika Kaunti ya Kilifi kwa sababu ya madhara ambayo tulikuwa tumeona wakati huo na kwa sasa sio Kilifi tena bali Pwani yote,” akasema Bi Ali.

Mwanaharakati wa maswala ya kijamii Bw Hamisi Njiwa amemtaka Rais Ruto kuingilia kati na kusuluhisha mzozano unaondelea, akisema kuwa huenda ukazua vita vikali vya ukabila na uhasama wa kisiasa.

Mwenyekiti wa Baraza la Viongizi wa kidini kaunti ya Kilifi Askofu Amos Lewa na Sheikh Famau Famau, waliongoza wenzao katika kupinga muguka.

[email protected]