Malala atatoboa? Chuma cha Cleophas ndani ya UDA kinavyozidi kupashwa moto
KATIBU Mkuu wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala anaonekana kujikaanga kwa matamshi na maamuzi yake ambayo yamemfanya ashambuliwe na wengi wanasiasa wa chama hicho.
Baadhi ya maafisa wa chama wanasema tayari anapigwa darubini na huenda akavuliwa wadhifa huo ambao amekuwa akishikilia kwa mwaka mmoja na miezi miwili tu.
Bw Malala ambaye wakati mmoja alikuwa diwani wa bunge la kaunti ya Kakamega na baadaye akawa seneta wa kaunti hiyo, kwa muda mrefu amekuwa akivurugana na baadhi ya wanachama wa UDA.
Lakini matukio ya Alhamisi wiki hii yanaonyesha kwamba huenda ametofautiana na wengi wao.
Mwanasiasa huyo mwenye ulimi mkali aliingizwa katika UDA na Rais Ruto Machi 2023 kutoka chama cha Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi cha Amani National Congress (ANC), baada ya kushindwa katika uchaguzi wa ugavana kaunti ya Kakamega.
Hata akiwa ANC, Bw Malala alikuwa akisumbuana na maafisa wa chama. Nusura atimuliwe katika chama hicho baada ya kutofautiana na Bw Mudavadi.
Alipojiunga na UDA, Malala alianza kuzua mawazo ya kuunganisha vyama tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza kuwa chama kimoja na hata akatoa makataa ya Agosti mwaka jana.
Aidha, alitaka ateuliwe kuketi katika Baraza la Mawaziri kama alivyokuwa akifanya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju.
Lakini hakufurahisha baadhi ya vyama tanzu vya Kenya Kwanza hasa ANC na Ford Kenya cha Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, kwa kushinikiza vivunjwe huku akivitaja kama vyama vya kijijini.
“Nilijiulu ANC kwa sababu nilitaka kuonyesha njia watu wangu wa ANC. Nilitaka kuwaonyesha uongozi. Kama vile Yohana Mbatizaji, nilikuja kuwaandalia njia. Hatimaye watakuja kuunganisha na kupata makao huku kwa urahisi. Nilijiuzulu na kujiunga na UDA ili kupatia ANC imani kwamba, kuwa na chama kimoja sio wazo baya,” Malala aliambia Taifa Leo katika mahojiano ya awali.
Lakini mambo yamemgeuka Malala katika chama tawala. Mnamo Alhamisi usiku, alisambaza video akilalamika jinsi alivyopoteza udhibiti wa ukurasa rasmi wa Facebook wa chama cha UDA.
Alidai kuwa ukurasa huo ulikuwa umedukuliwa na watu wasio wanachama wa afisi ya UDA.
Hii ni baada ya kutoa taarifa ambapo aliahirisha uchaguzi wa chama katika maeneo bunge ya kaunti ya Pokot Magharibi, uamuzi ambao maafisa wengine wa chama walipuuza na ambao kwa kawaida wanafaa kuwa chini yake kwa kuwa ndiye msemaji wa chama.
Duru katika chama hicho ziliambia Taifa Leo kwamba, wasimamizi wa ukurasa wa Facebook wa UDA ambao ni wandani wake, walivuliwa majukumu yao Alhamisi usiku kufuatia amri kutoka juu.
Habari hizi zilithibitishwa na Mwanamikakakati wa Mawasiliano katika Ikulu Dennis Itumbi, ambaye alipuuza madai kwamba ukurasa huo ulidukuliwa.
“Kurasa za UDA ziko salama katika mitandao yote ya kijamii, puuzeni yeyote anayesema jambo tofauti. Kuhusu masuala ya uchaguzi wa UDA, mpuuzeni Malala. Ni Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi inayoweza kutoa taarifa kuhusu uchaguzi,” alisema Itumbi, mwandani wa karibu wa Rais Ruto.
Bw Malala ambaye hakujbu maswali yetu kuhusu masaibu yake katika UDA ametofautiana na wanasiasa wa chama tawala akiwemo Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi.
Amekemea hata mawaziri kama Moses Kuria na Kipchumba Murkomen akiwataka wakome kushiriki siasa au wajiuzulu.