Habari za Kitaifa

Madaraka Dei: Wafanyabiashara, wakulima wa miwa wavuna

June 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA JESSE CHENGE

WAKENYA kwa maelfu kutoka kote nchini wametenga muda kuhudhuria sherehe za kitaifa za Madaraka Dei katika uwanja wa Masinde Muliro-Kanduyi, Kaunti ya Bungoma.

Sherehe hizo ni za 61 tangu Madaraka Dei ya kwanza mnamo Juni 1, 1963.

Rais William Ruto aliongoza sherehe za Jumamosi, ambazo pia zilihudhuriwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, mwenzao wa Seneti Amason Kingi, magavana wakiongozwa na Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka na wabunge na wageni wengine mashuhuri.

Soma Pia: Rais Ruto aongoza Wakenya kwa makala ya 61 ya Madaraka Dei

Mfanyabiashara Ben Wafula wa kutoka mji wa Bungoma, alisema kuwa sherehe za Madaraka zimeinua biashara yake kwa wiki kadha tangu matayisho hadi kilele.

“Biashara imekuwa ikiendelea vizuri kwa majuma matatu yaliyopita. Tumeshuhudia Wakenya kutoka maeneo mengine ya nchi wakifurika Bungoma na maeneo ya karibu huku wakinunua bidhaa na huduma kutoka kwetu,” akasema Bw Wafula.

Aidha, Bw Wafula alitaja Maonyesho ya Kilimo yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Kibabii kama fursa adimu kwa wakulima na wafanyabiashara katika eneo hilo, kwani mbinu mpya za kilimo zilionyeshwa katika maonyesho hayo.

“Wakulima walielimika kuhusu njia mpya za kilimo, kuongeza thamani kwa bidhaa na mavuno na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Mkulima Barasa Joseph kwa upande wake alimpongeza Rais kwa kuchagua kuandaa sherehe za Madaraka Dei katika Kaunti ya Bungoma.

Bw Barasa pia alimtaka Rais kuhakikisha kwamba mpango wa Bungoma kufanywa kuwa jiji unatimizwa.

Kuhusu malipo ya wakulima wa Nzoia, Bw Barasa alimshukuru Rais, ambaye kwenye hotuba aliahidi kuboresha sekta ya kilimo cha miwa si tu Bungoma, bali Kenya yote.

Wakulima wa miwa Nzoia wamekuwa wakidai malipo yao ya asilimia 20 iliyobaki.

Rais alisema serikali itafuta madeni ya Sh110 bilioni ya sekta ya sukari.

“Tunataka wakulima wa miwa wawe wakilipwa mara baada ya kufikisha miwa katika viwanda. Pia tunataka kuona wakulima wa miwa wakipata bonasi kama wenzao wa majanichai,” akasema Rais Ruto.

Dkt Ruto alitangaza serikali itatoa Sh600 milioni za kuimarisha mbegu ya miwa na kuleta utaratibu wa wakulima kulipwa mara miwa inapofikishwa kwa viwanda.

Tangu Alhamisi, Rais alizindua miradi mingi katika Kaunti ya Bungoma.

Alizindua ofisi ya idara ya uhamiaji na pasipoti, mradi wa bwawa la Kapkara huko Sirisia, taasisi ya mafunzo ya ufundi katika eneo la Webuye Magharibi na uzinduzi wa uimarishaji wa barabara ya Mayanja-Bisunu-Sirisia kuwa ya lami.

Sherehe za Jumamosi zilikamilika saa sita na nusu.

Kuanzia saa nane na nusu, kutakuwa na mechi kati ya klabu ya AFC Leopards na Nzoia Sugar.

Rais atakamilisha ziara yake Bungoma mnamo Jumapili.

Maelezo zaidi na Hassan Wanzala