Michezo

Klabu Bingwa Ulaya: Opta yawekea Real Madrid kichwa dhidi ya Borussia Dortmund

June 1st, 2024 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Real Madrid wanapigiwa upatu wa kutia kapuni taji la 15 la Klabu Bingwa Ulaya watakapovaana na Borussia Dortmund katika fainali ya msimu 2023-2024 ugani Wembley jijini London, Uingereza, Jumamosi kuanzia saa nne usiku.

Kompyuta maalum ya Opta inawapa washindi wa mataji mengi ya Klabu Bingwa Ulaya, Real Madrid (14) uwezekano wa asilimia 55.4 kupepeta mabingwa wa mwaka 1997 Dortmund katika muda wa kawaida ambao ni dakika 90.

Ubashiri huo unaungwa mkono pia na takwimu ambazo zinaonyesha kuwa Real wamelemea Dortmund mara sita, kutoka sare mara tano na kupoteza mechi tatu tu katika 14 wamekutana katika historia yao ya dimba hilo la kiwango cha juu kabisa barani Ulaya.

Vijana wa kocha Carlo Ancelotti hawajapoteza mechi katika Klabu Bingwa Ulaya msimu huu. Wakipata kuzima Dortmund, Los Blancos basi watakuwa mara yao ya kwanza kabisa kukamilisha msimu mmoja wa Klabu Bingwa Ulaya bila kupoteza katika historia yao.

Walikung’uta Union Berlin 1-0 (Septemba 20), Napoli 3-2 (Oktoba 3), Braga 2-1 (Oktoba 24), Braga 3-0 (Novemba 8), Napoli 4-2 (Novemba 29) na Union Berlin 3-2 (Desemba 12) katika makundi.

Madrid kisha walibandua Leipzig kwa jumla ya mabao 2-1 katika raundi ya 16-bora baada ya kuwachapa 1-0 (Februari 13) na kutoka sare 1-1 (Machi 6) na kupiga breki mabingwa wa 2022-2023 Manchester City katika robo-fainali kwa njia ya penalti 4-3 baada ya mkondo wa kwanza kutoka 3-3 (Aprili 9) na wa pili 1-1 (Aprili 14).

Mabingwa hao wa Uhispania walitinga fainali baada ya kutoka 2-2 dhidi ya Bayern Munich mnamo Aprili 30 na kucharaza miamba hao wa Ujerumani 2-1 Mei 8 katika nusu-fainali.

Dortmund walishinda mechi tatu, kutoka sare mara mbili na kupoteza mechi moja wakimaliza juu ya Kundi F lililokuwa pia na PSG, AC Milan na Newcastle United kabla ya kubandua PSV Eindhoven 3-1, Atletico Madrid 5-4 na PSG 2-0 katika usanjari huo.

Vikosi vitarajiwa (11 wa kwanza):

Real Madrid – Courtois, Carvajal, Nacho, Rudiger, Mendy, Valverde, Camavinga, Kroos, Bellingham, Vinicius Jr, na Rodrygo.

Dortmund – Kobel, Ryerson, Schlotterbeck, Hummels, Maatsen, Sabitzer, Can, Sancho, Brandt, Adeyemi, na Fullkrug.