Wezi wa mananasi ya Del Monte waonywa watakipata cha mtema kuni
NA MWANGI MUIRURI
KAMISHNA wa Murang’a Bw Joshua Nkanatha ametangaza rasmi katika Madaraka Dei kwamba wizi wa manasi Del Monte hautavumiliwa.
Mnamo Mei 24, 2024, serikali ya Kaunti ya Murang’a ilionya ingeanza kuwakabili wezi wa mananasi ya kampuni ya Kimarekani ya Del Monte. Onyo hilo lilitolewa Rais William Ruto akiwa katika ziara rasmi nchini Amerika ambapo alituzwa mavuno kemkem ya ushirikiano mwema.
Bw Nkanatha alitoa onyo kali kwa genge la wizi wa mananasi dhidi ya kampuni ya Kimarekani ya Del Monte akiliahidi cha mtema kuni.
Kampuni hiyo hushiriki kilimo cha mananasi katika Kaunti ya Murang’a ndani ya shamba la ukubwa wa zaidi ya ekari 20,000.
Akiongea katika maadhimisho ya Madaraka Dei ambayo yalikuwa ya kusherehekea miaka 61 ya uhuru, Bw Nkanatha alisema “genge hilo lielewe kwamba hatuna mzaha nalo kwa sasa na tutamulikana kwa hali zote”.
Haya yanajiri siku tatu baada ya maafisa wa polisi kukabili genge hilo kwa risasi katika Mji wa Makenji na Kabati, madai yasiyothibitishwa yakiarifu kuwa watu wawili waliaga dunia.
Bw Nkanatha alisema kwamba “hili ni taifa la utiifu kwa sheria na hakuna vile tutakaa kimya huku tukiwa na wachache ambao kazi yao ni kunyemelea mali ya washirika wetu wa kimaendeleo”.
Vita dhidi ya genge hilo vimechacha baada ya Rais William Ruto kufanya ziara rasmi nchini Marekani ambako inaashiriwa kwamba mahangaiko ya kampuni hiyo kupoteza takribani Sh5 Milioni kwa wiki ndani ya wizi huo yalijadiliwa.
Mabalozi wa Amerika hapa nchini wamekuwa wakiandaa mikutano ya kusaka suluhu la wizi huo na inadadisiwa kwamba huenda Rais Joe Biden akamsukuma Rais Ruto kusaidia kulipa Del Monte afueni.
Kampuni hiyo ya Del Monte huajiri zaidi ya watu 3,000 na huweka mabilioni ya pesa katika uchumi wa nchi kupitia ushuru, malipo ya ununuzi na pia miradi ya kijamii.
Bw Nkanatha alisema kwamba “huu utundu wa Vijana na wafanyabiashara kuungana na kugeuza kampuni hiyo kuwa uwanja wa wizi utakoma kwa vyovyote vile”.
Katika siku za hivi karibuni, kilio kimekuwa kikitanda kwamba walinzi wa kampuni hiyo huua vijana wa genge hilo la wizi.
Madai hayo yamekuwa yakitumika na soko la dunia kuweka vikwazo vya ununuzi wa bidhaa za Del Monte huku nayo mashirika ya haki za kibinadamu zikiwasilisha kesi mahakamani.
Mapema mwaka 2024, kampuni hiyo ilifuta walinzi wake wote 250 na kusajili wengine wa kampuni ya G4s lakini hali haikubadilika huku wizi hata ukizidi.