Vazi la hando lilivyochonga shepu ya mwanamke Mmijikenda
NA KALUME KAZUNGU
TOFAUTI na mtindo wa masoshiolaiti kuendea tiba na upasuaji wa kuongezea ukubwa wa makalio, mtoto wa kike wa Kimijikenda, hasa yule wa jamii ya Kigiriama, miaka kabla ya uhuru alikuwa anajiamini kwa vazi aina ya hando.
Hando ni vazi la Kimijikenda (Giriama) ambalo huvaliwa na kina mama na wasichana.
Aghalabu kuvalia hando huwa kwahitaji leso, kanga au kaniki.
Hando linapovaliwa hujumuisha matumizi ya uzi wa konge au wowote mzito ambao husaidia kufunga au kutundika vazi hilo kiunoni mwa mwanamke au msichana.
Vitambaa vya leso au kanga vinavyotumiwa kuunda hando hukunjwa ili vazi lenyewe liwe fupi kufika magotini.
Vazi la hando miongoni mwa Wamijikenda (Wagiriama) lilikuwa muhimu sana hasa katika kuichonga shepu ya mwanamke, hivyo kuufanya muonekano au umbile lake kuwa la kupendeza na kuvutia hata zaidi.
Mshirikishi wa Wazee wa Kaya Ukanda wa Pwani, Johnson Kitsao Ndokolani analitaja hando kuwa kitambulisho halisi cha tamaduni, mila na desturi za jamii ya Wamijikenda Pwani.
Bw Ndokolani anafafanua kuwa mavazi ni njia mojawapo ambayo waja wafaa kutumia hasa kutunza utamaduni wao.
Anasema miongoni mwa mavazi ambayo jamii ya Wamijikenda hutumia kuhifdhi mila na desturi za Pwani ni hando.
Anasisitiza haja ya vazi la hando, ambalo ni la wanawake, kulindwa kwa minajili ya vizazi vijavyo.
Anasema licha ya kudumu kwa miaka na mikaka, vazi hilo bado linaheshimiwa na kuenziwa na wengi.
Shepu ya chupa
“Hando ni vazi muhimu sana kwetu. Wanawake wetu walichongwa kishepu na hili vazi la hando. Yani ni kupitia hili vazi ambapo warembo wetu walipewa shepu ya chupa au figure-eight,” akasema Bw Ndokolani.
Alisema wazee wa Pwani tayari wanaendeleza mikakati ya kuona kwamba mavazi ya kitamaduni, ikiwemo hando yanalindwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa ili yasiangamie, kutoka kizazi hadi kingine.
Ikumbukwe kuwa kizazi kipya (cha sasa) kimekuwa kikilitelekeza sana vazi la hando huku wakiibukia sana fasheni za kileo, hivyo kuliweka katika hatari ya kuangamia.
“Twajivunia hando na mavazi mengine asilia ya Kimijikenda. Na ndio sababu tuko mbioni kuibuka na mikakati ya kutunza mavazi yetu, ikiwemo kutoruhusu kuigwa na kuvaliwa kivivi hivi na kila mtu, hasa endapo hujaruhusiwa au kupasishwa na wazee kufanya hivyo,” akasema Bw Ndokolani.
Alifichua kuwa baraza la wazee wa Kimijikenda tayari wameandika barua wanayonuia kuiwasilisha kwa Spika wa Bunge la Kilifi, Bw Teddy Mwambire hivi karibuni ili kuwepo na uwezekano wa bunge hilo kujadili na kuibuka na mswada wa sheria utakaodhibiti mavazi ya Kimijikenda.
Moneni Kahunda, mkazi wa Malindi, Kaunti ya Kilifi, alisema yeye hujihisi kutositirika ipasavyo kila mara anapokosa kuvalia hando.
Bi Kahunda katika aushi yake amekuwa akienzi sana kuvalia hando akiwa nyumbani au hata akiwa safarini.
Anasema kila anapovalia mavazi ya kisasa, ikiwemo sketi au rinda huwa hayuko huru ikilinganishwa na wakati anapovalia hando.
“Mimi nilianza kuvaa hando nikiwa miaka mitano. Nyanyangu mzaa baba, Bi Hawe Dzendere Kache ndiye aliyeanza kunivalisha hilo hando. Nikalizoea hadi sasa. Siko huru. Hujihisi uchi nikivalia mavazi ya kileo. Hando kwangu mimi ndo kusema. Pia hunipa shepu nzuri kama uonavyo,” akasema Bi Kahunda.
Mzee Joseph Kahindi alisema kuvalia hando humpa mwanamke wa Kimijikenda hadhi ya aina yake.
Anasema kinyume na ulimwengu wa sasa ambapo baadhi ya wanawake wamekuwa wakivalia mavazi nusu uchi, vimini nakadhalika, hando lilimuonyesha au kumwashiria mwanamke kuwa mtu wa nidhamu licha ya vazi hilo kuwa fupi kwa kiwango fulani.
“Ukilinganisha muonekano wa mwanamke aliyevalia hando lililofika magotini na yule aliyevalia kimini, utapata kwamba ni tofauti. Yule wa hando huheshimika zaidi kushinda wa kimini. Yaani hando ni nguo ya nidhamu licha ya ufupi wake,” akasema Bw Kahindi.
Kimsingi, vazi la hando linastahili kuwa refu hadi magotini ili kusitiri sehemu za siri kama njia ya kuonyesha heshima.
Mavazi ya kileo ya nusu uchi
Mbali na vipande vya leso au kanga, vazi hili pia hutengenezwa na pamba na huvaliwa kila mahali.
Wakati mwingine, hando pia huvaliwa wakati wa sherehe maalum.
Kuna aina ya hando iitwayo bandika, ambayo huwa fupi kuliko hando la kawaida na huwa na rangi nyingi. Bandika huvaliwa nyumbani na katika densi.
Vazi hili kadhalika husaidia mabinti kunengua viungo na kuonyesha sehemu za mwili kama vile paja.
Hata hivyo, mwanamke anapoenda pahala panapohitaji heshima, anastahili kuvaa leso juu ya bandika.
Kila rika la wanawake laweza vaa hando lakini kuna masharti kulingana na aina ya rangi.
Kwa mfano, hando nyeupe linaitwa bafuta na linatumika harusini bila masharti ya rika.
Aina nyingine za hando ni lile la msimbiji (ramsimbiji) ambalo huwa rangi ya samawati.
Pia kuna hando la kaputula (rakaputula) ambalo aghalabu huwa ni fupi na lenye rangi tofauti tofauti.
Isitoshe, hando huvaliwa na mapambo mengine kama vile tunda, vivorodete, mkufu, tsango, vidanga na vifufu.
Kutokana na hadhi au taadhima ya hando, mpiganiaji maarufu wa uhuru chini Kenya kutoka jamii ya Wamijikenda, Bi Mekatilili wa Menza alivaa, kulithamini na kulienzi sana vazi la hando katika maisha yake.