Mfungwa wa ubakaji aliyetoroka akitibiwa anyakwa tena
NA MERCY KOSKEI
MFUNGWA Stanley Cheruyot,29, ambaye anatumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumnajisi mtoto, amekamatwa tena baada ya kutoroka kutoka Hospitali ya Rufaa ya Nakuru.
Cheruyot alikamatwa mjini Molo Jumatatu saa nne usiku baada ya kutoroka hospitalini alipokuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji.
Kamanda wa Polisi Kaunti ya Nakuru Bw Samuel Ndanyi, akithibitisha kukamatwa kwake, alisema kuwa Cheruyot alitiwa mbaroni na polisi baada ya kupokea habari kutoka kwa wananchi.
“Tukio la mfungwa kutoroka hospitalini liliripotiwa katika kituo cha polisi cha Kaptembwo. Ilichukua juhudi za maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kushirikiana na polisi kutoka Nakuru na Molo kumsaka na kumkamata. Tayari amekabidhiwa kwa idara ya magereza,” Bw Ndanyi alieleza.
Cheruyot, ambaye alikuwa anatumikia kifungo chake katika Gereza Kuu la Nakuru, alitoroka kutoka Hospitali ya Rufaa ya Nakuru Jumatatu asubuhi, alipokuwa anasubiri kufanyiwa upasuaji wa mkono.
Inaaminika kuwa alikamatwa katika eneo la Keep Left mjini Molo, akiwa amevaa nguo za kiraia na kubeba sare za gereza kwenye mfuko wa karatasi.
Cheruyot vilevile alipatikana na simu ya mkononi ambayo inaaminika mawimbi yake yalisaidia katika juhudi za kumsaka na kumkamata.
Anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kutoroka gerezani.