Akili Mali

Bee smoker: Mtambo wa kisasa katika uvunaji asali

June 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

NI rahisi kuvuna asali kutoka kwa mizinga ya kisasa, kinyume na changamoto za awali wakati wa kurina asali kutoka kwa mizinga ya kienyeji.

Hii ikiashiria kwamba ukuaji wa teknolojia mwanzo umefanya iwe rahisi kwa wafugaji wa nyuki kwa kuzingatia mbinu sahihi za ufugaji, mazingira na hatimaye kujiongezea kipato.

Rachel Munovi mmoja wa wakurugenzi wa Bee Farmers Hub eneo la Karen, Kaunti ya Nairobi, anasema, siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la mahitaji ya bidhaa zinazotokana na nyuki kama vile asali.

Himizo

Ndiposa kumekuwa na kampeni nyingi za kuwahimiza wakulima katika sekta ya ufugaji wa nyuki kuzingatia mifumo ya kisasa ili kuvuna asali kitaaluma.

Isitoshe ili kuzingatia usafi wa hali ya juu mkulima anapaswa kuzingatia mfumo sahihi wa uvunaji kwa kutumia mtambo spesheli wa smoker.

Mtambo wenyewe unaweza kuagizwa kutoka mataifa ya nje au vilevile kutengenezwa humu nchini.

Matumizi yake ni mepesi na utamhakikishia mkulima usalama wake binafsi asije akang’atwa wakati wa kurina asali.

Anasema hii ni ala ambayo hutumika kufukiza moshi kwenye mizinga ya kisasa ili kuwafanya nyuki watulie kwa muda.

Moshi wenyewe kwa kawaida huwa hauna madhara kwa nyuki ila huwapoza makali na kuwafanya watulie shughuli ya kuvuna inapoendelea.

Kwa upande mwingine huwasaidia wafanyakazi katika shamba la ufugaji wa nyuki kuwa na wakati mwepesi kwa kuepuka ajali ambazo zinaweza kutokea shambani.

Ni mtambo ambao umeundwa kwa aina maalum ya chuma kisichoshika kutu.

Sehemu ya chini huwa na uwazi ambapo ndipo shinikizo la hewa hutokea pindi mkulima anapobonyeza.

Presha yenyewe inatosha kufikisha moshi katika sehemu ya juu.

Anasema aina nyingi ya matawi ya majani au mseto wa makapi zinaweza kutumika kwenye mtambo wenyewe ila mkulima achukue tahadhari asije akawafukuza nyuki kutoka kwenye mzinga.

Kwa upande mwingine Bi Rachel anasema hii inaweza kuwa fursa nyingine ya ajira kwa vijana kwani wanaweza kujitosa katika usambazaji wa makapi au majani yanayotumika ndani ya smoker.

“Ndani ya smoker majani huteketea taratibu na makali ya moto huendelea kuongezeka kadri mkulima anavyoendelea kuongeza presha,” asema.
Hata hivyo anawashauri wakulima wasijisahau yaani wavalie magwanda maalum kama vile mabuti na glavu.

Elimu ya kutosha

Mtambo wenyewe ni rahisi kutengeneza kwa matumizi ya wakulima vijijini almuradi wapate elimu ya kutosha kutoka kwa wataalam wa kuunda zana za nyuki kibiashara

Ameendelea kuambia Akilimali kwamba hii ni njia mojawapo ambayo mkulima anaweza kutumia kujipiga msasa ili kubaini anatumia mbinu sahihi kuvuna asali safi kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

“Unapodumisha usafi wakati wa kuvuna asali ndivyo unavyoambulia asali ya hadhi ya juu na kuwavutia wateja kutoka viwandani ambao huchukua amazao yako kwa bei nzuri,” asema.

Aidha kupitia teknolojia ya kutumia smoker, wafugaji nyuki wanaweza kujifunza mambo mengi kama vile namna ya kutunza mazingira kwani nyuki wanahitaji mazingira safi.