Mwanachuo aliyerekodiwa akimpiga afisa wa polisi ashtakiwa kwa wizi wa mabavu
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Kiufundi (TUK) ambaye video yake ilisambaa katika mitandao ya kijamii tangu Juni 2 ikionyesha akimtandika afisa wa polisi ameshtakiwa kwa wizi wa mabavu katika mahakama ya Milimani.
Hata hivyo, Ian Ngige Njoroge aliyepata umaarufu kwa kumshambulia afisa wa polisi alieleza hakimu mwandamizi Ben Mark Ekhubi kwamba “alipata kichapo cha mbwa alipotiwa nguvuni na maafisa wa polisi na anahitaji matibabu ya dharura.”
Ngige mwenye umri wa miaka 19 alikana mashtaka sita mbele ya mahakimu Bw Ekhubi na hakimu mwandamizi mahakama ya kuamua kesi za trafiki Martha Nanzushi. Alikana kuvuruga wenye magari katika barabara ya Kamiti katika eneo la njia panda la Mirema kaunti ya Nairobi.
Mbele ya Ekhubi, alikabiliwa na shtaka la kumnyang’anya kimabavu Koplo Jacob Ogendo simu ya mkononi aina ya Samsung ya thamani ya Sh50,000 na betri ya redio ya mawasiliano ya polisi.
Alishtakiwa pia kumpiga na kumjeruhi Koplo Ogendo na kukataa kutiwa nguvuni.
Mbele ya Nanzushi, mshtakiwa alikana kuwavuruga watumiaji wengine wa barabara kwa kugeukia katikati ya barabara, kubeba abiria watano badala ya abiria wanne kwenye gari lake KDJ 207P na kukaidi agizo apeleke gari lake kituo cha polisi cha Kasarani usiku wa Juni 2, 2024 mwendo wa saa mbili usiku.
Mawakili Duncan Okatchi, Suyianka Lempaa na Ken Echesa walieleza mahakama Ngige, “anashtahili kupewa medali ya kitaifa kwa kukataa kutoboka hongo na kusimama kidete na kutetea haki.”
Mawakili waliomba agizo litolewe apelekwe Hospitali Kuu ya Kenyatta kupokea matibabu kutokana majeraha aliyopata kwa polisi.
Mawakili hao pia waliomba korti ikatae ombi la Polisi kumzuilia mshtakiwa kwa siku tatu wakiendelea kurekodi taarifa za mashahidi.
Kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki alimsihi hakimu aamuru mshtakiwa azuiliwe kwa siku tatu katika kituo cha polisi kuwezesha afisa anayechunguza kesi hiyo akamilishe uchunguzi.
Ombi hilo lilipingwa vikali na mawakili Okatchi, Lempaa na Echesa wakisema “watesi wa mshtakiwa kamwe hawapasi kuruhusiwa kumzuilia kwa siku nyingine tatu kwa vile jambo baya zaidi litatendeka.”
Bw Okatchi alisema polisi walimtesa mshtakiwa na kumtandika na kumjeruhi.
Aliomba korti imwachilie kwa dhamana kwa vile anaishi na wazazi wake.
“Mshtakiwa huyu anavyosimama mbele ya hii mahakama ni mhasiriwa wa kichapo cha polisi. Amejeruhiwa. Ameumizwa. Nguo alizovaa akiwa korokoro ya polisi zimelowa damu. Polisi walirekodi video na kutuma katika mitandao ya kijamii nguo hizo zikiwa zimelowa damu,” Bw Okatchi alimweleza hakimu.
Pia wakili huyo alicheza ukanda wa video uliorekodiwa na polisi wakimhoji mshtakiwa huku wakisikika wakimtusi na “kumwita Ng’ombe na Mbwa.”
Bw Okatchi alisema Kifungu nambari 29 (c),(d) na (e) cha Katiba kinasema kwamba mshukiwa yeyote asidhalilishwe ama kuteswa kimwili na kisaikolojia.
Alisema polisi walimtesa mshtakiwa na “sasa wanaomba siku nyingine tatu kumtesa zaidi. Je, mshtakiwa atarudi akiwa hai?”
Hakimu alielezwa polisi walimtia mshtakiwa nguvuni akiwa kwa wazazi wake na “hapo walimtandika hadi akazirai mara mbili.”
Mabw Lempaa na Echesa walisema kifungu cha sheria nambari 296(2) cha sheria za uhalifu ambacho Ngige ameshtakiwa kiliharamishwa 2016 na majaji watatu wa mahakama kuu.
Majaji hao walimpa Mwanasheria Mkuu miezi 18 kuwasilisha hoja bungeni kufutiliwa mbali sheria nambari 295,296 na 297 za sheria za uhalifu kwa vile zinakinzana na Katiba.
“Hakuna shtaka halali mbele ya mahakama kwa vile sheria 296(2) iliharamishwa na mahakama,” Bw Lempaa alisema huku akidai Mwanasheria Mkuu, Polisi na Wabunge wamezembea katika kazi zao.
Hakimu aliruhusu polisi wamzuilie mshtakiwa kwa siku moja hadi Juni 5, 2024.
Bw Ekhubi aliagiza mshtakiwa azuiliwe katika gereza la Viwandani na kuamuru apelekwe Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) kupokea matibabu ya dharura.
Hakimu alimruhusu mzazi mmoja wa Ngige aandamane naye KNH.
Bi Nanzushi alimwachilia mwanafunzi huyo kwa dhamana ya Sh60,000 pesa tasilimu katika kesi ya trafiki.