Maoni

MAONI: Wakati wowote Ruto na Gachagua watakorofishana, Wakenya ndio watafaidi

June 5th, 2024 2 min read

NA LEONARD ONYANGO

WAZEE kutoka maeneo ya Bonde la Ufa na Mlima Kenya wameanza juhudi za ‘kuwapatanisha’ Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.

Inaonekana wazee hao wamejitwika jukumu hilo baada ya Bw Gachagua kujitokeza hadharani na kuwafokea wandani wa Rais Ruto anaodai kuwa wanamhujumu.

Hata hivyo, Bw Gachagua amekuwa akisitiza kwamba hamna uhasama baina yake na Rais Ruto ambaye mgogoro uliopo unatishia kupasua chama chake cha United Democratic Alliance (UDA).

Japo wapo wanaodai kuwa uhasama baina ya viongozi hao wawili unatishia umoja wa nchi, ukweli ni kwamba vita hivyo vina manufaa makubwa kwa nchi.

Vita hivyo vitaongeza upinzani nguvu hivyo basi kuusaidia kuzuia kupitishwa kwa sheria zinazokandamiza raia bungeni.

Upande wa serikali una idadi kubwa ya wabunge ambao wamekuwa wakipitisha kiholela sheria bila hata kutathmimi manufaa yake kwa raia.

Mwaka jana, Wakenya waliachwa vinywa wazi wabunge wa eneo la Mlima Kenya walipokiri kuwa walipitisha bila kusoma Mswada wa Fedha wa 2023.

Walipitisha mswada huo uliopingwa vikali na Wakenya ili kufurahisha Rais Ruto bila kuzingatia masilahi ya wapigakura waliowachagua.

Wabunge wa Mlima Kenya walilazimika kukiri kwamba hawakusoma mswada huo baada ya kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa wakulima wa eneo hilo waliolia kwamba sheria iliwaumiza kwa ushuru wa juu.

Tayari wabunge wanaoegemea upande wa Bw Gachagua wameapa kupinga vikali baadhi ya mapendekezo katika Mswada wa Fedha wa 2024 ambao utawatwika Wakenya mzigo mzito wa ushuru.

Mswada huo unapendekeza kuongeza ushuru wa bidhaa muhimu kama vile mkate.

Pendekezo jingine ambalo limezua joto ni kuwataka wamiliki wa magari kulipa ushuru kila mwaka.

Ikiwa wandani wa Bw Gachagua wataungana na Upinzani kupinga mswada huo, Wakenya watakuwa na afueni kubwa.

Uhasama baina ya wandani wa Rais Ruto na Bw Gachagua ni sawa na vita vya panzi ambavyo huwa furaha kwa kunguru.

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alipokosana na naibu wake, Dkt Ruto mara baada ya uchaguzi wa 2017, chama tawala cha Jubilee kililazimika kusaka msaada wa upinzani ili kupata uwezo wa kupitisha miswada muhimu.

Dkt Ruto alifanikiwa kuvutia upande wake zaidi ya wabunge 70 hivyo ilikuwa vigumu kwa serikali kupitisha miswada Bungeni.

Upinzani unafaa kushirikiana na Bw Gachagua ili kuhakikisha kuwa miswada inayopitishwa Bungeni inazingatia masilahi ya raia na wala si kwa manufaa ya wachache serikalini.

Wabunge wa upinzani wasisaliti raia kwa kupitisha miswada ambayo itaumiza raia.