Habari za Kitaifa

Tusipokonywe afya, kaunti zalia

June 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

MABILIONI ambayo Sekta ya Afya imetengewa huenda yakazua tumbojoto huku serikali kuu na zile za kaunti zikionekana kung’ang’ania sekta hiyo.

Huku zikisalia siku chache tu kabla ya Bajeti Mpya kusomwa, Baraza la Magavana (CoG) limeishutumu serikali kuu kwa kula njama ya kupokonya kaunti sekta ya afya kwa kuzisawiri kama zilizoshindwa kusimamia na kulipa madeni yanayodaiwa sekta hiyo muhimu.

Magavana wakiongozwa na Mwenyekiti wa CoG, ambaye pia ni Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga Bi Anne Waiguru, wamelalamika kwamba bado hawajapokea fedha za matumizi kutoka kwa Hazina Kuu kwa muda wa miezi mitatu, kiasi cha zaidi ya Sh100 bilioni, huku bajeti ya 2023-2024 ikikamilika.

Mwenyekiti wa CoG na Gavana wa Kaunti ya Tharaka Nithi Muthomi Njuki ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Magavana kuhusu Afya, wamesema, hata baada ya kuchelewesha fedha, serikali kuu imekuwa ikitumia vyombo vya habari kueneza dhana kwamba kaunti zimekosa kulipa madeni ambazo zinadaiwa na Shirika la Kusambaza Dawa Nchini (Kemsa).

Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM) Kipengee 17 (6) 2012 inasema kuwa “Hazina Kuu, mwanzoni mwa kila mwezi, na katika tukio lolote lisilo baada ya tarehe 15 kutoka mwanzo wa mwezi, itasambazia serikali za kaunti fedha za matumizi ya mwezi unaofuata.”

Huku mfumo Jumuishi kuhusu Habari za Usimamizi wa Fedha (IFMIS) ukiripotiwa kujikokota kuanzia Juni 15, wakuu wa kaunti wameelezea wasiwasi wao kuhusu malimbikizo ya miezi mitatu ambayo hawajapokea.

Kulingana na Gavana Njuki, ripoti kuhusu madeni ambayo kaunti zinadaiwa na Kemsa, zinaashiria njama za kuzisawiri vibaya kaunti.

“Kama serikali kuu ingekuwa inazingatia sheria na kutupatia rasilimali zetu tarehe 15 kila mwezi, hakuna kaunti ambayo ingekuwa na deni la Kemsa,” alisema gavana Njuki.

“Deni si mbaya. Tuna mkataba na Kemsa unaoruhusu kaunti muda wa malipo wa siku 90. Huo ni muda sawa na kipindi ambacho kaunti hazijapokea mgao wao wa mapato,” akaongeza.

Suala hili limeibua mgogoro ambao umekuwa ukitokota kuhusu juhudi za baadhi ya maafisa serikalini kurejesha baadhi ya sekta muhimu ikiwemo afya chini ya serikali kuu badala ya kaunti kama ilivyokuwa kabla ya Katiba Mpya 2010 kubuniwa.

Wakuu wa kaunti, hata hivyo, wamesimama imara wakisisitiza yaliyofanikishwa kupitia ugatuzi.

Gavana Njuki ametoa wito kwa serikali kutimiza ahadi yake ya Sh2 bilioni kwa Kemsa ili kuimarisha shirika hilo huku akisema kaunti ziko tayari kulipa madeni yote inayodaiwa na Kemsa mara tu zitakapopokea mgao wa fedha.

Serikali 47 za Kaunti zinatazamiwa kupata mgao wa Sh400.1 bilioni katika bajeti mpya itakayoanza kutumika Julai baada ya Kamati ya Pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuafikiana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti, Ndindi Nyoro, akihutubia vyombo vya habari majuzi alisema wameufanyia marekebisho makuu mswada unaohusu ugavi wa mapato.

“Hii inaashiria kuwa tunasema na kutenda na tunamaanisha kuimarisha ugatuzi. Fedha hizi zinamaanisha huduma zaidi katika sekta za afya, kilimo na elimu ya chekechea,” akasema Bw Nyoro.