Wito majukumu ya Uhuru na Gachagua yatofautishwe
NA MWANGI MUIRURI
BARAZA la Wazee Mlima Kenya sasa linataka majukumu ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na yale ya Naibu Rais Rigathi Gachagua yawekwe wazi na yalainishwe kwa mujibu wa utamaduni wa jamii husika ili kukomesha mgongano wa aina yoyote.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu Bw Wachira Kiago, Bw Kenyatta ndiye mfalme wa jamii za Mlima Kenya kwa kuwa katika vigezo vyote vya ujasiri, uadilifu na kujituma kwa niaba ya jamii hizo, hakuna mwingine aliye hai kwa sasa ambaye anampiku rais huyo wa zamani.
Alisema kwamba wakati wa ghasia za mwaka 2007/08 ambapo Bw Kenyatta alichangia kufa kupona usalama wa watu wa asili ya Mlima Kenya katika maeneo mengi ya Rift Valley na Nairobi, ni kigezo kimoja kikubwa sana katika kuafikia hadhi yake ya ufalme.
“Bw Kenyatta alisimama na jamii hizi katika dhiki ya ghasia hizo za baada ya matokeo ya kura za urais ambazo ziliishia hata wengine kuteketezwa hadi kufa hata walipokuwa wametafuta hifadhi kanisani,” akasema Bw Kiago.
Alisema majuto ya watu wa Mlima Kenya ni kwamba “licha ya hayo yote, aliitwa mnajisi na muuaji na akashtakiwa katika mahakama ya uhalifu dhidi ya binadamu (ICC) iliyoko nchini Uholanzi”.
Katika hali hiyo, Bw Kiago alisema Bw Kenyatta anabakia kuwa shujaa wa kijamii na anayefaa tuzo ya mfalme wa kijamii.
Naye mfadhili mkuu wa baraza hilo Bw Kung’u Muigai ambaye pia ni binamuye Bw Kenyatta, aliambia Taifa Leo kwamba ufalme huo wa Bw Kenyatta unafaa kuwa na mipaka ya upenyo wake ndani ya siasa za eneo na za nchi kwa niaba ya jamii za Mlima Kenya.
“Licha ya kuwa Bw Kenyatta amehitimu kuwa mfalme wa kijamii, inafaa ieleweke wadhifa huo huwa na majukumu ambayo mshikilizi hupewa kutekeleza katika jamii. Bw Kenyatta ndiye anafaa kuwa na kijiti cha mamlaka ya ufalme (Muthigi wa Uthamaki) huku naye Bw Gachagua akiwa na kile kijiti cha uongozi (Muthigi wa Utongoria),” akasema Bw Muigai.
Alifafanua kwamba kijiti cha Bw Kenyatta hadi sasa ni kile cha uongozi “kwa kuwa hatujakitekelezea lile tambiko ambalo ni la kukipaka mafuta ya baraka ili kiwe kijiti cha ufalme”.
Bw Muigai alisema kwamba hadi sasa katika jamii za Mlima Kenya, kuna vijiti viwili vya ufalme ambavyo vilikuwa kwanza, mikononi mwa baba mwanzilishi wa taifa Mzee Jomo Kenyatta na pili, kwa Rais mstaafu marehemu Mwai Kibaki.
“Bw Kenyatta (Uhuru) alirithi kijiti cha uongozi kutoka kwa Kibaki mwaka wa 2013 na hadi sasa hicho ndicho amekuwa nacho na ambacho baada yake kustaafu na eneo la Mlima likawa na Bw Gachagua ambaye ndiye wa cheo cha juu, kwa utaratibu na desturi za kijamii, Bw Kenyatta anafaa kuachana na majukumu hayo ya uongozi na atwikwe yale ya ufalme,” akaeleza.
Bw Kung’u alisema mkwaruzano ulioko Mlima Kenya kwa sasa kuhusu nafasi ya Bw Kenyatta na Bw Gachagua inatokana na hali ya rais huyo mstaafu kukataa kupanda ngazi hadi kuwa mfalme huku aking’ang’ania kuwa kiongozi wa kijamii.
“Kwa kawaida, mfalme wa kijamii anafaa kuwa mshauri na mwenye kukata kesi za migogoro ya kijamii. Naye kiongozi anafaa kuwa wa kushauriwa na mfalme ili aipeleke jamii katika vita vya uhasama na pia vya kuweka mikataba ya masilahi. Katika vikao vya mfalme na kiongozi, kijiti cha ufalme ndicho hutamalaki huku kile cha uongozi kikiwa kimelala chini,” akasema.
Alisema kwamba katika historia ya Agikuyu, “hatujakuwa na wakati ambapo tulikuwa na mgogoro kama wa sasa kwa kuwa Mzee Kenyatta aliaga dunia 1978 akiwa hana mpinzani wa ufalme huku naye Kibaki akichukua nafasi yake kama mshauri wa kijamii pasipo kumsumbua Bw Kenyatta aliyemrithi mwaka wa 2013”.
Hili lina maana kwamba iwapo Bw Kenyatta atakubali kuwa mfalme wa jamii za Mlima Kenya, basi katika familia yao kutakuwa na vijiti viwili vya ufalme, hali ambayo hulifanya boma la Hayati Kenyatta kuwa la hadhi.
Pia, boma hilo lina marais wawili wa Kenya ambao ni mzee Kenyatta na Uhuru, ikimaanisha pia uwepo wa mama taifa wawili ambao ni Mama Ngina Kenyatta na Mama Margaret Kenyatta (wote wawili walipata jina moja la ubatizo la Margaret).
Bw Muigai alisema kwamba “ni wakati huu sasa ambapo tunaona jamii ikiwa na viongozi wawili ambao wanatekeleza ushindani wa uongozi na ambapo wa kulaumiwa ni sisi wazee na pia Bw Kenyatta kwa kukosa kuweka zile adabu za kimsingi za mamlaka kwa mujibu wa tamaduni zetu”.
Bw Kung’u alisema kwamba kile sasa kinafaa kufanywa ni mkutano wa dharura wa kumwagiza Bw Kenyatta achukue majukumu yake ya Ufalme na Bw Gachagua achukue yake ya uongozi ndio kuwe na amani ya kijamii.
Iwapo hilo litafanyika, Bw Muigai alisema kwamba Bw Kenyatta atapigwa marufuku ya kushiriki siasa za uchaguzi akibakia tu kutoa ushauri katika kikao cha wadau kuhusu mwelekeo wa jamii hiyo kuchukua kuhusu siasa.
Aidha, alisema kwamba maamuzi yote ya kisiasa ambayo vikao vya wadau vitaafikia kuhusu mwelekeo wa kisiasa, vitatekelezwa kwa sasa na Bw Gachagua.
“Huo ndio ulikuwa utengano wa 2022 baada ya Bw Kenyatta kukosa kuandaa kikao cha wadau ili kuafikiana mkondo wa kijamii kuhusu siasa. Yeye alikimbia kuunga mkono Bw Raila Odinga pasipo maafikiano, naye Bw Gachagua akakimbia kuunga mkono Dkt William Ruto pasipo maafikiano. Kwa bahati, Bw Gachagua alishinda karata hiyo na kwa sasa hatuna budi kulainisha mikakati yetu ya kijamii na Bw Kenyatta achukue wajibu wake huku Bw Gachagua akibakia na uongozi ndio sasa tuanze kuganga yetu ya 2027 na 2032,” akasema Bw Muigai.