Ombi la hakimu kutambulika mjane wa kachero John Njoroge lakataliwa
NA MWANGI MUIRURI
SAFARI ya hakimu wa Milimani-Nairobi, Bi Irene Ruguru Ngotho ya kuomba mahakama imsaidie kutambulika kama mrithi wa mali ya aliyekuwa mkuu wa mikakati katika kitengo kilichoogopwa na wengi cha Flying Squad marehemu John Njoroge imefika ukingoni kwa kukataliwa.
Njoroge aliaga dunia mnamo Machi 8, 2024.
Njoroge alikuwa mzawa wa familia ya wadosi wa polisi kwa kuwa alikuwa ni nduguye aliyekuwa mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Joseph Kamau kati ya 2004 na 2006.
Baada ya Njoroge kuaga dunia, Bi Ngotho alizuka kama uyoga na kuzima juhudi za mazishi yake akisema kwamba alikuwa ni mke wake mwendazake japo kwa uhusiano ambao haukuwekwa wazi lakini alikuwa ameahidiwa ndoa kabla ya kuaga dunia.
Bi Ruguru alifanikiwa kuzima maandalizi ya mazishi ya mwendazake kupitia agizo la mahakama kabla ya kesi kutamatika mnamo Aprili 30, 2024, ambapo Jaji HK Chemitei alitoa uamuzi kwamba kesi ya mwenzake wa mahakama ndogo, haikuwa na mshiko ya kisheria.
Katika stakabadhi zake za kortini za kudai atambulike kama mke wa marehemu Njoroge, hakimu Ruguru alisema kwamba alikuwa akiishi na mwendazake katika mtaa wa Jacaranda ulio katika eneobunge la Roysambu, Kaunti ya Nairobi.
Alisema kwamba yeye ndiye alikuweko wakati Njoroge alikumbwa na matatizo ya kiafya na akamkimbiza hadi katika hospitali na kama mke mwema, akatia saini stakabadhi muhimu za kulazwa hospitalini.
Baada ya Njoroge kuaga dunia, Bi Ruguru alikimbia mahakamani kusaka utambuzi akidai kwamba familia ya kwanza ya mwendazake ilikuwa inamkana hivyo basi kukiuka haki zake za kimsingi na pia za mtoto aliyekuwa tumboni mwake.
Alishikilia kuwa mtoto huyo aliyekuwa tumboni alikuwa damu ya Njoroge hivyo basi kumpa uhusiano wa moja kwa moja kama maharusi.
Alisema licha ya kutokuwa na watoto pamoja, alikuwa ameshika mimba tatu na ambazo ziliishia kuharibika lakini kwa jaribio la ukingoni mwa uhai wake Njoroge, Bi Ruguru akawa amefanikiwa kumweka mimba nyingine na iliyoishia kuzaliwa kwa mtoto wao baada ya mauti kumnasa.
Aidha, Bi Ruguru alitetea kesi yake kwa dhati akisema kwamba walikuwa pia wanapanga kufanya harusi rasmi katika siku za baadaye kidogo.
li kuyapa maneno yake uzito, hakimu huyo alisema kwamba hata mwendazake alikuwa akimjengea nyumba ya ndoa katika uwanja ulioko eneobunge la Juja, Kaunti ya Kiambu.
Bi Ruguru alisema katika stakabadhi za kesi kwamba “familia ya mwendazake ilikuwa inalenga kumhadaa kupitia kumtambua kama mke wa mwendazake lakini asiyekuwa na haki ya kumrithi”.
Mnamo Aprili 15, 2024, mahakama ilitoa mwelekeo kwamba “kesi ya Bi Ngotho ilikuwa hafifu na ikaelekeza kwamba kijana wa mwendazake aliyetambuliwa kama Peter Kamau, apewe idhini ya kumwandalia babake mazishi”.
Bi Ruguru alikata rufaa mara moja akiitaka mahakama ielekeze kwamba wajane wa mwendazake watambuliwe kama Bi Irene Ruguru na pia Bi Anne Nduku ambaye ndiye familia ilikuwa ikimtambua kama mkwe wao.
Rufaa hiyo iliishia Jaji Chemitei kudadisi kwamba “wawili hawa walikuwa wamekaa pamoja kwa muda mchache sana kiasi cha kutotambulika kisheria kama uhusiano wa ndoa”.
Jaji Chemitei alisema kwamba msingi wa kesi ya hakimu Ruguru ilikuwa kwamba “mwendazake ndiye baba mtoto ambaye alizaliwa baada ya kifo chake na pia alikuwa akimjengea nyumba wakingojea kuoana katika siku za baadaye hali ambazo kamwe haziwezi zikatafsiriwa kuwa ndoa”.
Baada ya uamuzi huo, familia ya mwendazake ilichukua tu siku moja na ya pili ambayo ilikuwa Mei 1, 2024, akazikwa katika Kaunti ya Murang’a alikokuwa amejinunulia shamba.
Asili ya mwendazake ni Kaunti ya Kiambu.
Ripoti ya familia ya mwendazake ya Machi 8, 2024 ilisema kwamba “Njoroge aliaga dunia akipokezwa matibabu katika hospitali ya Aga Khan Jijini Nairobi baada ya kuugua ugonjwa wa nimonia”.
Ilimtaja mwendazake kama “muadilifu, mkarimu, mpenda watu na utu na aliyekuwa kiungo thabiti cha ustawi wa kijamii katika mashinani”.
Aliendesha operesheni kali alipokuwa hai. Alikuwa na mchango muhimu polisi aliokuwa akiwaongoza walipomkamata daktari bandia Mugo wa Wairimu katika mtaa wa Githurai 44 mwaka wa 2018 ambaye baadaye alipatikana na hatia ya kuwapooza wanawake waliofika kwake kutibiwa na kuishia kuwabaka wakiwa hoi.
Mnamo Novemba 21, 2022, Mugo alihukumiwa kifungo cha miaka 29 gerezani baada ya kupatikana na hatia.
Maafisa waliofanya kazi na mwendazake katika uhai wake walimtaja kama mchangamfu na pandikizi la mtu ambaye kwa ujasiri mkuu alikuwa anatumia nguvu alizokuwa amejaliwa kuwafunga pingu wahalifu wasumbufu.
Ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu hudai alikuwa anatumia nguvu kupita kiasi.
Familia ya kachero Kamau ilimuomboleza mwendazake ambaye ni mzawa wa Murang’a ikimtaja kama mwadilifu, mkarimu, mpenda watu na mwenye utu.
Ilisema alikuwa kiungo thabiti cha ustawi wa kijamii mashinani.
Mnamo mwaka 2017 Kamau anakumbukwa kama afisa aliyepambana sana na vurugu za mrengo wa upinzani–CORD– jijini Nairobi baada ya uchaguzi mkuu mwaka huo.
Lakini mwendazake pia mnamo mwaka 2007, alihusishwa na kutoweka kwa aliyekuwa naibu kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Kimani Ruo ambaye hadi leo hajawahi kupatikana. Ukweli wa kilichotokea haujafahamika hadi sasa.