Habari za Kaunti

Wabunge wa Nairobi wapinga ubomoaji wa nyumba kiubaguzi

June 6th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE kutoka maeneobunge yaliyoko Kaunti ya Nairobi wanapinga shughuli ya ubomoaji wa nyumba na mijengo mingine kando ya mito.

Wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nairobi Bi Esther Passaris, wabunge hao wamemtaka Rais William Ruto kuamuru kusitishwa kwa ubomoaji huo, hadi mpango madhubuti kuhusu ulipaji fidia na kuwatafutia makao mbadala waathiriwa utakapowekwa.

Isitoshe, wabunge hao wamelalamika kuwa shughuli hiyo inaendeshwa “bila utaratibu maalum, kwa upendeleo na kwa njia inayokiuka haki za waathiriwa”.

“Majengo hayafai kuwepo katika maeneo yanayokaribiana na mito na yanafaa kubolewa. Lakini wale ambao nyumba zao zinabomolewa wanafaa kupewa notisi, kuonyeshwa pa kuenda na kulipwa ridhaa kwa sababu serikali ndio iliidhinisha nyumba hizo kujengwa,” Bi Passaris akasema bungeni mnamo Jumatano alipokuwa akichangia hoja kuhusu Bajeti ya Ziadi ya Pili.

“Kwa sababu imebainika kuwa serikali haijaweka mpango kama huu, Rais Ruto asitishe shughuli hiyo. Kinachotuudhi sisi kama viongozi wa Nairobi ni kwamba shughuli hiyo haiendeshwi kwa njia ya utu kwa sababu mali za watu zinaharibiwa kiholela na mitaa wanakoishi maskini ndio inalengwa huku ile ya matajiri ikizaswa,” akaongeza.

Kwa upande wake Mbunge wa Dagoreti Kaskazini Beatrice Elachi, alihoji ni kwa nini nyumba za kifahari zilizojengwa ukingoni mwa mito katika mitaa ya Kileleshwa, Runda na Lavington haibomolewi.

“Mbona ubomoaji huu umekita katika mitaa wanakoishi maskini kama vile Mathare, Mukuru, Ruaraka, Kibera na Kariobangi? Mbona ubomoaji huu hauendeshwi katika mitaa ya kifahari kama Kileleshwa na mingineyo? Si huu ni ubaguzi?” Bi Elachi akauliza.

Mnamo Jumatano Mbunge wa Starehe Amos Mwago aliomba taarifa kutoka kwa Wizara ya Ardhi na Wizara ya Usalama wa Ndani kuhusu mantiki ya ubomoaji huo.

Bw Mwago ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Jubilee, alisema kuwa nguvu kupita kiasi zinatumika katika ubomoaji huo, hali inayowaongezea raia madhila zaidi.

“Nataka wenyeviti wa wizara hizi mbili kutoa maelezo kuhusu ni kwa nini maafisa wanaoendesha shughuli hii wanatumia nguvu kupitia kiasi na kuishia kuwajeruhi wananchi na kuharibu mali zao. Mbona wananchi hawapewi notisi ya kuhama kabla ya matingatinga kuletwa kuanza ubomoaji?”, akauliza.

Kauli ya Bw Mwago iliungwa mkono na wenzake Mark Mwenje (Embakasi Magharibi), Babu Owino (Embakasi Mashariki) na T J Kajwang wa Ruaraka.

Kulingana na agizo lililotolewa na serikali, majengo yaliyoko umbali wa mita 30 kutoka kingo za mito yanafaa kubomolewa kama hatua ya kuzuia maafa yaliyoshuhudiwa wakati wa mvua ya masika kati ya Aprili na Mei 2024.

Lakini Mbw Kajwang’ na Mwenje wanadai kuwa katika baadhi ya maeneo, hata nyumba zilizoko umbali wa mita 60 kutoka kingo za mito zinabomolewa.

“Ikiwa nyumba zilizo umbali wa mita 60 kutoka kwa mito zinabomolewa, basi watu wote watafurushwa kutoka eneobunge langu la Ruaraka. Ubomoaji huu unafaa kusitishwa kwa sababu unaendeshwa kinyama na bila mpangilio maalum,” mbunge huyo akasema.