Habari za Kitaifa

Wakazi wa mitaa ya mabanda wapinga Mswada wa Fedha wa 2024

June 7th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

WANACHAMA wa vuguvugu la The Social Justice Movement (TSJM) Alhamisi walifanya maandamano nje ya Majengo ya Bunge kuwahiza wabunge kuzima nyongeza za ushuru zilizopendekezwa kwenye Mswada wa Fedha wa 2024.

Wakiongozwa na mshirikishi wao, Bw Wilfred Olal, wanaharakati hao ambao ni wakazi wa mitaa ya mbalimbali ya mabanda Nairobi, waliwataka wabunge kusaka njia mbadala za kuisadia serikali kuongeza mapato yake zisizoumiza raia maskini.

“Wakati kama huu ambapo gharama ya maisha ingali juu, serikali haifai kuongeza ushuru wa bidhaa za kimsingi kama mkate, mafuta ya kupikia na huduma nyinginezo. Kwa kuongeza ushuru kwa bidhaa hizi. Serikali itakuwa ikiumiza familia ambazo tayari zinazongwa na ukosefu wa ajira, miongoni mwa changamoto nyinginezo,” Bw Olal akasema.

Mswada huo unapendekeza ushuru wa ziada ya thamani (VAT) ya kima cha asilimia 16 kwa mkate, ushuru wa asilimia 2.5 kwa magari yote, nyongeza ya ushuru wa mafuta ya kupikia yanayoagizwa kutoka ng’ambo kutoka asilimia 10 hadi asilimia 20, miongoni mwa aina nyingine za ushuru.

Wakati huu, Kamati ya Bunge kuhusu Fedha inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani inaendesha vikao vya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa umma kuhusu mswada huo ambapo wadau wengi wamepinga mapendekezo ya kuongeza ushuru.

Vuguvugu la TSJM pia limewataka wabunge kuendesha uchunguzi kuhusu ubomoaji wa majengo karibu na kingo za mito inayopitia mitaa ya mabanda kwa kutozingatia haki za binadamu za wakazi.

“Tunawataka wabunge kuchunguza shughuli hii inayoendeshwa kinyama ili wale wanaoitumia kama kisingizio cha kuendeleza mauaji na uharibifu wa mali ya raia masikini wachukuliwe hatua za kisheria,” Bw Olal akasema.

Taarifa yenye malalamishi ya kundi hilo ilipokewa na wabunge Samuel Atandi (Alego Usonga) na Babu Owino (Embakasi Mashariki).

Waliwahakikishia kuwa wataongoza kampeni kali Bungeni ya kuhakikisha kuwa Mswada wa Fedha wa 2024 unafanyiwa marekebisho kuondoa ushuru unaowaumiza raia.