Jamvi La Siasa

Gachagua, Uhuru na Raila waingia zizi moja

June 7th, 2024 4 min read

NA MWANGI MUIRURI

HATUA ya kinara wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga kujitokeza hadharani kuunga mfumo wa ugavi rasilimali za taifa kwa kuzingatia idadi ya watu imezua wasiwasi miongoni mwa wandani wa Rais William Ruto kwamba kuna muungano wa kumpinga ambao unasukwa.

Hii ni kwa sababu kauli ya Bw Odinga inawiana na ile ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pamoja na Naibu Rais Rigathi Gachagua, huku wadadisi wa masuala ya kisiasa sasa wakitazamia kwamba kuna muungano wa kisiasa unaonukia kati ya hao watatu.

Hali hiyo inajitokeza wakati utawala wa Rais Ruto uko chini ya shinikizo kuu kwamba ubuni njia za kujipendekeza kwa Wakenya kwa kuwa, kwa mujibu wa kura za maoni, wengi wamechoka nao.

Ni katika taswira hiyo ambapo kujitokeza kwa hali ambayo inaashiria kuundwa kwa mrengo ulio na uwezo wa kumng’oa Rais Ruto mamlakani katika uchaguzi mkuu wa 2027, kunaonekana kuzua msisimko wa kisiasa.

“Kwa kiwango kikuu, siasa husukumwa na dhana. Taswira za matukio ndizo hutoa utabiri wa baadaye. Kwa hili la ugavi wa rasilimali, usifikirie kuwa ni kitu kidogo. Hili ni tukio kubwa mno la kisiasa,” asema mdadisi wa masuala ya kisiasa Mlima Kenya, Prof Ngugi Njoroge.

Prof Njoroge anasema kwamba wakati Bw Kenyatta na Bw Gachagua wanaonekana kuwa katika mrengo mmoja kuhusu suala fulani, kuna uwezekano mkubwa wa Mlima Kenya kuungana kwa asilimia karibu 100.

“Ukiwaongeza sauti ya Bw Odinga, basi hiyo ni kauli ambayo huwezi ukaipuuza na ni lazima tujiulize Rais Ruto anasimama wapi katika mjadala. Ama yuko kwa kina hao watatu (Gachagua, Kenyatta na Odinga) au yuko kwingineko, Hizo ndizo siasa za udadisi,” asema.

Anaongeza, “Sio lazima udadisi huo uwe wa uhakika lakini huwa muhimu kwa kuzua mijadala ya kisiasa na kusaidia katika kuafikia maamuzi.”

Mshauri mkuu wa Rais Ruto kuhusu masuala ya kiuchumi Dkt David Ndii anaupinga kwa dhati mfumo huo akiutaja kuwa wa kusaidia walio wengi kuwanyanyasa walio wachache.

“Aidha, mfumo wa aina hiyo utasaidia maeneo ambayo yako na rotuba na uwekezaji wa juu wa rasilimali za umma kuzidisha manufaa, nao wale wa maeneo yaliyotengwa tangu uhuru wa taifa wakizidi kusononeka,” asema Dkt Ndii.

Swali linalojitokeza ni kuhusu msimamo wa Dkt Ruto katika mjadala huo wa ugavi wa rasilimali ikiwa mshauri wake mkuu wa kiuchumi anapinga hadharani kupitia maandishi na pia ulimi wake.

Isitoshe, ni hali ambayo imeonekana kama ndio inazua wasiwasi kwamba kuna mkono fiche ambao unachochea siasa za utengano Mlima Kenya kwa kuwa wandani wengi wa Rais Ruto wanapinga mfumo huo.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti, amekuwa kimya kuhusu mjadala huo licha ya kwamba ni mmoja wa wanaopendekezwa kuwa wafaafu kwa wadhifa wa Bw Gachagua 2027.

Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria ni mwingine ambaye katika siku za hivi karibuni amejiunga na wanaopinga mjadala huo, akisema kwamba “vile viti tuko navyo ndani ya serikali hii vinatosha kutuwezesha kuwapelekea watu wetu Mlimani maendeleo mengi”.

Lakini Bw Gachagua anasema kwamba wanaopinga na wasio na msimamo katika eneo la Mlima Kenya kuhusu suala hilo ni wasaliti.

Katika siasa za kujumlisha kura, mrengo unaounga mfumo huo wa ugavi rasilimali kwa kuzingatia idadi ya watu utakuwa na ufuasi mkuu katika kaunti zilizo na zaidi ya watu 1 milioni.

Kaunti hizo ni Nairobi, Kiambu, Nakuru, Kakamega, Bungoma, Meru, Kilifi, Machakos, Kisii, Mombasa, Uasin Gishu, Narok, Kisumu, Migori, Murang’a, Homa Bay, Kitui, na Kajiado.

Hofu ya Dkt Ndii ni kwamba “hizi ni kaunti 18 pekee na swali ni kuhusu zile nyingine 29”.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni ambaye ni mwandani wa Bw Kenyatta, anasema kwamba wao hawapendekezi yeyote apoteze mgao wake alio nao kwa sasa.

“Kile tunasema ni wale ambao wamekuwa wakipata mgao usioambatana na idadi yao waongezewe,” asema Bw Kioni.

Hali hiyo, kwa mujibu wa aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi, inatoa msukumo mwingine kuhusu ushuru kwa kuwa ukipendekeza gharama zaidi kwa taifa, basi ujiandae kutafuta ushuru wa kufadhili.

Bw Ngugi anasema kwamba hesabu ya haki ni wale ambao wamekuwa wakipata pesa nyingi kuliko idadi yao, wapunguziwe na ikabidhiwe waliokuwa wakipata mgao hafifu.

Hata hivyo, Bw Ngugi anaonya kwamba huu ni mjadala ambao utazua cheche nyingi sana za kisiasa na kiuchumi kiasi cha kusababisha hata uhasama wa kijamii.

Anaongeza kwamba hata magavana wenyewe katika kaunti hizo zinazodai mgao kwa idadi ya watu, hawajapata mbinu ya kugawa rasilimali za kaunti kwa kuzingatia idadi ya watu.

“Kwa mfano kwetu Murang’a, maeneobunge ya Kangema na Mathioya husemwa ni madogo sana na yanafaa kuunganishwa. Katika mgao wa Hazina ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NG-CDF), huwa tunapata mgao sawa katika maeneobunge yote saba ya Murang’a. Katika hali ya mfumo wa ugavi rasilimali kwa msingi wa idadi ya watu, maeneobunge hayo mawili yanafaa kupunguziwa na ndio sababu kwa mfano, mbunge wa Kangema Bw Peter Kihungi anaupinga,” asema Bw Ngugi.

Anasema kwamba Kaunti ya Murang’a kwa sasa iko na wadi 35 na ambazo kila mojawapo hupokezwa Sh9 milioni na Gavana Irungu Kang’ata pasipo kuzingatia zilizo na watu wengi na zilizo na wachache “hivyo basi kukupa taswira ya ugumu ulioko katika kuafikia mfumo huo wa ugavi wa rasilimali”.

Bw Ngugi anaongeza kwamba wakati mjadala huo utaanza kushika kasi, maeneo mengi ambayo yanajiorodhesha kama yaliyotengwa na yanayolengwa kupunguziwa pato yataamka na kupinga.

“Suala hili likifika hapo, siasa za nchi zitaanza kuwa na kelele nyingi,” asema.

Bw Ngugi anachukulia mjadala huo kama uchokozi wa moja kwa moja kwa utawala wa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt Ruto ndio uyumbe na uanze safari yake mapema ya kufunga virago kuelekea nyumbani.

“Mlima Kenya hautaki kusikia jingine isipokuwa mgao kwa idadi. Wafuasi wa Bw Odinga huwa wanangojea tu wamsikie amesema waelekeze bidii zao wapi na lao liwe ni kufuata tu pasipo kubishana. Sasa ni wakati wa Rais naye kutangaza msimamo wake ndio tujue bendera inafuata upepo wa wapi. Kwa uhakika, huu mjadala sio mchezo na sio rahisi na uko na uwezo wa kubadilisha ulingo wa kisiasa kwa njia kuu,” akasema.

[email protected]