Watunzaji mazingira walia tatizo ni wachafuzi vichwa ngumu
NA KALUME KAZUNGU
LAMU hushuhudia harakati nyingi za watunzaji wa mazingira wanaojitolea kuokota chupa za plastiki na kusafisha miji na fuo za Bahari Hindi.
Hii ni kwa sababu taka nyingi, hasa zile za plastiki hutupwa kiholela katika maeneo hayo.
Tabia hiyo ya kuchafua mazingira ni mbaya kwani huwa ni yenye kuathiri maisha ya binadamu na pia ya viumbe wanaoishi baharini.
Baadhi ya watunzaji wa mazingira waliohojiwa na Taifa Leo hata hivyo waliilaumu jamii ya Lamu kwa kile wanachokitaja kuwa ni kiburi cha wazi.
Mwanamazingira wa Lamu Bw Ahmed Swaleh, alisema hakuna ambacho wananchi hawakijui kuhusiana na madhara ambayo plastiki inaweza kusababishia viumbe hai wa baharini.
Kulingana na Bw Swaleh, wakazi wamepokezwa mafunzo mengi lakini baadhi yao wameamua kuwa vichwa ngumu.
Alieleza masikitiko yake kuona wananchi bado wakipuuzilia mbali elimu waliyopokezwa na mashirika kuhusu kudhibiti mazingira, hasa yale ya ufuoni.
“Tumewaelimisha watu kuepuka kutupa ovyo plastiki. Pastiki ni sumu kwa viumbe kama vile samaki ambao huishia kufa endapo watakumbana na plastiki nyingi kwenye mazingira yao. Yote hayo tumeyafundisha ila kuna walioamua kuendeleza tabia zao ngumu,” akasema Bw Swaleh.
Bi Khadija Abdalla, ambaye pia ni mtunzaji wa mazingira, alisema ulegevu wa wanajamii katika kupigania suala la mazingira safi na salama huchangia madhara.
Bi Abdalla alisema iwapo wananchi wenyewe wataungana na kupiga vita matumizi ya plastiki, Lamu litakuwa eneo shwari.
“Hapa Lamu hata haina haja ya sisi kushikwa shingo ndipo kudhibiti usafi wa mazingira yetu hasa yale ya baharini. Jamii hapa hutegemea uvuvi, kumaanisha endapo plastiki zitaendelea kuua samaki wetu, basi uchumi utadorora. Watu wajukumike kumaliza hili zogo la plastiki kwenye fuo zetu,” akasema Bi Abdalla.
Utafiti wa Hali ya Kimazingira ya Bahari uliofanywa na Kituo cha Kibiolojia cha Centre for Biological Diversity ulibaini kuwa maelfu ya wanyama, wakubwa kwa wadogo, kuanzia kwa nyangumi, huishia kufa katika hali mbaya baada ya kula au hata kujipata wamenaswa na plastiki baharini.
Kulingana na utafiti huo, samaki kwenye ukanda wa Pacific Kaskazini huishia kula kati ya tani 12,000 hadi 24,000 za plastiki kila mwaka, hatua ambayo husababisha majeraha kwenye matumbo yao na hatimaye vifo.
Hali hiyo pia inahofiwa kuishia kusambazwa kwa chembechembe za plastiki kutoka kwa samaki wadogo hadi kwa wanyama wengine (mamalia) na hata binadamu wanaokula samaki hao wadogo ambao kwa wakati fulani waliathirika na plastiki.
Maeneo kama Lamu, Kwale, Kilifi na maeneo mengine ya Pwani pia yameshuhudia kasa wakifa baharini baada ya kula plastiki au kunaswa na plastiki hizo.
Ni kutokana na ukweli huo ambapo wanamazingira hata wameibuka na mifumo mbadala ya kupigana nalo na kumaliza janga la taka za plastiki.
Miongoni mwa mbinu hizo ni ile ya kuokota taka za plasiki baharini, kuziongezea ubora na kisha kuzitumia upya tena kutengenezea bidhaa.
Ikumbukwe kuwa mnamo Januari 2019, Lamu iligonga vichwa vya habari ulimwenguni kote pale ilipoibuka na mashua ya kwanza kuwahi kutengenezwa kwa kutumia taka za plastiki zilizookotwa baharini.
Mashua hiyo inatambulika kwa jina FlipFlopi.
Isitoshe, wanamazingira wamekuwa wakiwahimiza wananchi kuokota na kukusanya taka za plastiki kisiwani Lamu na kisha kulipwa mwishowe.
Wanamazingira wa Lamu pia wamewahi kuunda viti kwa kutumia taka zilizookotwa baharini za plastiki.
Wanawake waliojitolea kudhibiti usafi wa mazingira kwenye miji kama vile Mkokoni, Lamu Mashariki pia wameshuhudiwa wakikusanya chupa za plastiki baharini ambapo walizitumia kujengea na hata kurembesha nyumba na vibaraza.
Mbali na hayo, kampeni mbalimbali za kuwahamasisha wakazi wa Lamu kuhusu athari za uchafuzi wa mazingira na umuhimu wa kudhibiti mazingira safi zimekuwa zikiendelezwa.
Kampeni hizo kilele chake kimekuwa ni makongamano ambayo yamekuwa yakiwaleta pamoja wanamazingira na wakazi katika ajenda moja ya kuhakikisha maeneo wanayoishi na pia mazingira ya baharini yanawekwa safi.
Licha ya watunza mazingira kuendeleza juhudi hizo karibu kila kukicha, changamoto bado ziko kwani kumeshuhudiwa plastiki zikisheheni, hasa kwenye fuo nyingi za Bahari Hindi Lamu.