Habari za Kitaifa

Mwanafunzi aliyeshtakiwa kumshambulia polisi aachiliwa kwa bondi ya Sh700,000

June 7th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu aliyeshtakiwa kwa kumjeruhi na kumwibia polisi simu yake na betri ya redio ya mawasiliano ya maafisa na kisha kukataa kukamatwa, ameachiliwa kwa bondi ya Sh700,000.

Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi alimwachilia huru Ian Ngige Njoroge baada ya kukaa rumande kwa siku tano.

Ngige alikanusha kuwa alimpiga Koplo Jacob Ogendo mnamo Juni 2, 2024.

Tukio hilo liliibua taharuki ya umma wakati video hiyo ilienea katika mitandao ya kijamii kueneza tukio hilo kama vile moto wa msituni.

Akimuachilia Ngige kwa dhamana, Bw Ekhubi alisema dhamana ni haki ya kikatiba kwa kila mshukiwa.

Alisema uzito wa kosa sio sababu madhubuti ya kuthibitisha kunyimwa dhamana ya mtuhumiwa.

Alieleza kuwa upande wa mashtaka ulipinga vikali dhamana ukisema makosa hayo yanavutia adhabu kali.

Bw Ekhubi alisema adhabu ya shtaka la kumshambulia mlalamishi kwa mabavu huwa hukumu ya kifo mshtakiwa akipatikana na hatia na kwamba kosa la kumsababishia mlalamishi majeraha adhabu yake huwa ni kifungo cha jela maisha.

“Uzito wa kosa sio sababu kuu ya kutaka mahakama kumnyima dhamana mshtakiwa,” aliamua Bw Ekhubi.