Lugha, Fasihi na Elimu

Machogu atuliza wanafunzi, wazazi kuhusu karo ya elimu ya juu

June 7th, 2024 1 min read

NA DAVID MUCHUNGUH

WANAFUNZI watakaojiunga na vyuo vikuu Agosti na Septemba watasubiri hadi Julai 31, 2024, ili kujua kiasi cha karo wanachohitajika kulipa.

Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu, ameeleza wanafunzi kwamba, hawatalipa karo yote iliyoorodheshwa katika barua zao za mwaliko bali watasubiri wasajiliwe ili kujua kiasi ambacho familia zao zitahitajika kulipa.

Wanafunzi na wazazi wamestaajabishwa na kiwango cha juu cha karo katika barua zao za usajili walizopewa na vyuo vikuu mbalimbali.

Karo iliyoorodheshwa kwa kila kozi pasipo kuzingatia ufadhili wa serikali ni kati ya Sh144,000 hadi Sh720,000 kila mwaka kutegemea na aina ya kozi na chuo walichoteuliwa kujiunga nacho.

“Serikali imegundua kuwa baadhi ya wazazi na walezi wanadhani watahitajika kulipa karo yote iliyonakiliwa kwenye barua za usajili. Karo kwa kila mpango itafadhiliwa kupitia vitengo vitatu ambavyo ni ufadhili wa elimu, mikopo na michango ya familia,” alisema Bw Machogu kupitia taarifa mnamo Ijumaa.