Maswali rapa maarufu Prezzo akikosa usaizidi mwafaka alipozimia jukwaani
NA FRIDAH OKACHI
MWANAMUZIKI nguli wa rapu Jackson Ngechu Makini almaarufu Prezzo alianguka na kuzimia wakati wa kutumbuiza mashabiki katika hafla ya The Bahati’s Empire, tukio ambalo limezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu taratibu za matibabu zilizotumika kuokoa maisha yake.
Furaha ya hafla iliyohudhuriwa na watu mashuhuri akiwemo Naibu Rais Rigathi Gachagua ilichukua mkondo wa ghafla wakati Prezzo alipoanguka chini akitumbuiza huku kiini cha kuanguka kwake kisijulikane mara moja.
Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha baadhi ya watu waliovalia suti wakikosa kufahamu mbinu huduma ya kwanza (First Aid) ya kuokoa maisha yake.
Usaidizi wa haraka uliotolewa na waliohudhuria huku wakingojea usaidizi zaidi wa kimatibabu, ulitiliwa shaka kwa kufanya visivyo.
Baadhi ya waokoaji walionekana wakimwekea kizuizi kwenye mdomo bila kufahamu tatizo lake.
Wakati huo huo, uzinduzi wa The Bahati’s Empire, hatua muhimu kwa mwanamuziki Bahati na familia yake, uliendelea kama ulivyopangwa.
Muuguzi katika hospitali ya Mbagathi Bi Lucy Nyokabi hata hivyo ameambia Taifa Leo huduma ya kwanza anayofaa kupewa mtu aliyeanguka na kuzirai.
Alisema kuwa kutoa nafasi ya hewa safi huwa ni jambo muhimu na kumpa muda aweze kurejea kimawazo.
“Jambo la kwanza, hakikisha mwathiriwa analala na upande. Pili, hakikisha hana nguo ambazo zinamshika kwenye mwili wake. Tatu, hakikisha anapata hewa safi ili aweze kurudi kwenye hali yake ya kawaida,” alisema Bi Lucy.
Anasema hufai kuweka vitu kwenye mdomo wake iwapo hufahamu hali yake ya afya.
Prezzo baadaye Ijumaa aliandika ujumbe kwenye akaunti yake ya Instagram, akisema alikuwa amepata nafuu na kwamba kilichomfanya kuzirai ni kuchok na kwamba kwa sasa atatumia muda wake kupumzika na kukaa karibu na familia.
“Kinyume na tetesi zilizozagaa mitandaoni kuhusu hali yangu ya afya, nataka kusema kwamba niko salama…si rahisi kuwa Rais (utani), Nimekuwa nikifanya kazi kwa bidii sana ndio maana nimechoka. Hongera kwa Bahati Mpire kwa kazi nzuri. Namshukuru Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuunga mkono sanaa…Nawapenda wo!” akahitimisha kwa kauli mbiu yake.