Habari za Kaunti

Wakulima wa kahawa Kirinyaga waandamana kulalamikia malipo duni

June 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA GEORGE MUNENE

MAMIA ya waandamanaji kutoka Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa cha Mutira kaunti ya Kirinyaga wamemwagika barabarani huku wakilalamikia malipo duni kwa mazao yao.

Wakulima hao waliandamana hadi katika afisi za shirika hilo na kuzifunga kwa nguvu.

Pia walivifunga viwanda vyote saba vya kusaga kahawa vinavyofanya kazi chini ya shirika hilo, wakiapa kuendelea kulemaza shughuli hadi malalamiko yao yatakaposhughulikiwa.

Kulikuwa na vuta nikuvute wakati wakulima hao wenye ghadhabu waliwakabili wafanyakazi wa shirika hilo, hali iliyolazimu wafanyakazi kutimua mbio kuokoa maisha yao.

Ilibidi polisi wa kuzima ghasia kuingilia kati ili kurejesha utulivu.

Wakulima hao wa kahawa wanalalamika kwamba walilipwa pesa chache mno kuliko kiwango ambacho walitarajia.

Walitaka chama hicho cha ushirika kuwapa maelezo.

“Hatuna furaha hata kidogo na ndio maana tumefunga afisi za chama hiki cha ushirika pamoja na viwanda vyote saba,” akasema mmoja wa wakulima wa kahawa katika eneo hilo.

Diwani wa wadi ya Mutira Bw Kinyua Wangui, alisema wakulima walitarajia kupokea malipo mazuri lakini wakakerwa mno na malipo duni waliopokea.

Alisema wakulima hao hawana imani na wasimamazi wa chama hicho cha ushirika.

Aidha, wakulima walioshiriki maandamano hayo waliapa kuwafukuza wasimamizi wakuu wa chama chao cha ushirika na kuwaweka wapya ikiwa hawatapata malipo wanayotaka.

“Tulitarajia kulipwa Sh128 kwa kila kilo moja ya kahawa lakini cha kushangaza tulipata kiwango chini na hicho. Hili halikubaliki,” mkulima mwingine akasema.

Wakulima hao waliambia wanahabari kwamba walitia bidii ya mchwa katika mashamba yao ya kahawa baada ya serikali kuwahakikishia kuwa wangepata malipo mazuri kutokana na kahawa yao.

“Juhudi zetu zimepotea bure. Tukiendelea kupokea malipo duni hata tutalemewa kulipa madeni ambayo tunadaiwa,” akasema mkulima mwingine aliyeshiriki maandamano hayo.