Oscar Sudi kuhojiwa kuhusu unyakuzi wa ardhi ya maskwota wa Ngeria
NA TITUS OMINDE
KAMATI ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ardhi imemwagiza mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, kujiwasilisha kwake ili kufafanua madai kwamba alihusika na mradi unaodaiwa kunyakua ardhi iliyodhamiriwa kuwapa makao maskwota wa Ngeria.
Maskwota hao wamewasilisha malalamishi kwa Kamati ya Bunge inayoshughulikia masuala ya Ardhi wakishutumu Chuo Kikuu cha Moi kwa kula njama na mbunge wa eneo hilo kuwafurusha kutoka ardhi hiyo yenye ekari zaidi ya 1,500 wanayodai kuishi zaidi ya miongo minne.
Katika kikao cha kamati hiyo Ijumaa, mjini Eldoret, Kamati ilimhoji Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Moi, Isaac Kosgey, viongozi eneo hilo na viongozi wa maskwota.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Mugirango Kaskazini, Joash Nyamoko na naibu wake, Mbunge wa Naivasha, Jayne Kihara, waliafikiana kwa pamoja kumwagiza Bw Sudi kujiwasilisha mbele ya Kamati hiyo katika muda wa siku saba.
Katika vikao hivyo, jina la Mbunge huyo wa Kapseret, Oscar Sudi, lilijitokeza bayana kwenye suala hilo.
Akizungumza baada ya ziara kwenye shamba hilo kubwa lenye ekari 1,515, Bw Nyamoko alithibitisha kuwa Kamati hiyo hivi karibuni itaagiza Bw Sudi ajiwasilishe ili kufafanulia Kamati.
“Tuna habari kuwa baadhi ya viongozi kutoka eneo hili wanahusika na kulima ardhi ya taasisi hii, lakini tutaweza kuthibitisha hilo. Tumewaagiza makarani wetu kuamua ili Oscar Sudi afike mbele ya Kamati kwa sababu alitajwa wakati wa kikao chetu,” alisema Bw Nyamoko.
Ardhi inayozozaniwa ipo kwenye bewa kuu la Chuo Kikuu cha Moi, Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu.
Kamati vilevile iliagiza shughuli zote za kilimo katika ardhi inayozozaniwa zisitishwe mara moja hadi uamuzi suala hilo lililowasilishwa Bungeni litakapotatuliwa.
Katika malalamishi yao, maskwota wamedai kuna njama za kuwafurusha katika shamba hilo ili kutoa fursa ya kulizia mwanasiasa eneo hilo kimagendo.
Wabunge wanachunguza madai ya kuwafurusha maskwota kwenye ardhi hiyo ikiwemo madai kuhusu unyakuzi wa ardhi ya umma.
Kamati hiyo ilimwangazia Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Moi, Prof Kosgey kuhusu madai ya kukodisha kinyume na sheria, nusu ya ardhi ya taasisi hiyo kwa shirika la kibinafsi la uwekezaji.
Ardhi iyo hiyo ambayo chuo kinadaiwa kukodisha kwa njia haramu ndiyo inayopiganiwa na maskwota wa Ngeria Estate walioripotiwa kufurushwa miaka ya 1980.
Kamati ilielezwa kwamba ardhi hiyo imelimwa na mwekezaji ambaye hakutajwa na kukodishiwa shirika kwa jina Cropsoko.
Maskota wakiongozwa na David Kemboi, James Chirchir na James Sitienei, wanadai walirithi ardhi inayozozaniwa kutoka kwa mababu zao kabla ya kuachwa bila makao walipofurushwa na kuirai Kamati iwasaidie kuirejesha.