Siasa

‘Betty e sawa’ adai baadhi ya viongozi Mlima Kenya ni kama fisi

June 8th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Betty Maina amedai kwamba kumezuka ‘team mafisi’ wa ulafi kisiasa eneo la Mlima Kenya.

Alisema kwamba “tuko hali mbaya na wanasiasa hao ambao licha ya kuwa na minofu ya mamlaka mdomoni, hata kabla waitafune na waimeze bado wanalia wawekwe minofu zaidi mdomoni”.

Akiongea katika eneo la Karugia alikohudhuria mazishi ya Bi Beth Wambui, Bi Maina alisema kwamba “ukiwasikiliza wengine wa Mlima Kenya wakiteta huwezi ukaamini eti wao ndio wako na asilimia 47 ya serikali”.

Bi Maina ambaye hufahamika kwa jina la majazi la ‘Betty e sawa‘ (Betty yuko sawa) alisema “wote ambao kwa sasa wako nyanjani wakisaka manufaa mengine ya kimamlaka kuliko yale tuliyo nayo ni sawa na fisi kwa ulafi”.

“Jamii nyingine zinashindwa kuelewa shida yetu ni gani kwa kuwa zinatuorodhesha kama walio ndani ya serikali na kwamba tunavuna manufaa kupindukia,” akasema Bi Maina.

Halafu akaongeza, “Wanapotusikia kila asubuhi tukiweka kwa meza shinikizo zaidi za kudai manufaa ya ziada, wanatuona kama wasioridhika kwa vyovyote vile.”

Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Betty Maina akiongea katika eneo la Karugia alikohudhuria mazishi ya Bi Beth Wambui. PICHA | MWANGI MUIRURI

Alisema Rais William Ruto anawekwa chini ya shinikizo licha ya kuwa amejitolea kutuza eneo hilo kwa wingi wa manufaa ya serikali kutokana na asilimia 87 ya kura zao walizompa.

“Mimi ukiniuliza msimamo wangu ni gani katika siasa hizo, nitajibu ya kwamba kuna haja ya viongozi wa kutoka eneo la Mlima Kenya kutosheka. Tukome kujipenda kupita kiasi na badala yake tuzingatie baraka kuu tuliyo nayo na tuwe watiifu kwa Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua ambao tunafaa kuwapa nafasi ya kutuongoza katika kuafikia kile muungano wa Kenya Kwanza uliahidi kutimizia Wakenya,” akasema.

Kwa sasa, siasa Mlima Kenya zimegeuka kuwa za mirengo, wengine wakidai pesa zaidi za maendeleo huku nao wengine wakisema wanataka mamlaka ya urais na unaibu wake katika uchaguzi wa mwaka 2027.

Wengine wanataka maeneobunge zaidi huku pia wengine wakisema wanataka nyadhifa zaidi serikalini.

Hali hiyo imegeuza eneo hilo kuwa ngome ya vichwa motomoto vya habari hasa kuhusu anayosema huku akipingwa Bw Gachagua, wafuasi wa Azimio wakizidisha kampeni zao nao wandani wa Rais Ruto wakipambana kumkinga dhidi ya shutuma.

Bi Maina alisema kwamba iwapo watakoma kujipenda kupita kiasi na kuelewe kwamba wao ni miongoni mwa jamii nyingi zinazounda taifa la Kenya, basi kutakuwa na usawa.

“Sisi wa Mlima Kenya tunapaswa kufahamu kuna wananchi wa maeneo mengine ambao nao wanasubiri kutimiziwa ahadi za mwaka 2022. Tupunguze hiki kilio cha tamaa na ulafi,” akarai.