Makala

Wenyeji wa Mpeketoni wasukuma kutengewa siku ya kupanda mti uliozaa mji wao

June 9th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, wameibua shinikizo za kutaka siku maalum itengwe ili kuutambua, kuuenzi, kuupanda na kuukuza mti wa Mpeketo.

Mnamo miaka ya sabini (1970s), Mwanzilishi wa taifa la Kenya Mzee Jomo Kenyatta alifika kwenye mojawapo ya maeneo ya Lamu yaliyotambulika kwa jina la asili kama Ziwa Mkunguya.

Ni hapa ambapo Mzee Kenyatta, katika harakati za kutafuta upepo mzuri wa kubarizi, alifikishwa kwenye mti mmoja kwa jina Mpeketo, ambapo alikaa chini ya kivuli chake na kupenda mandhari hayo si haba.

Ilimlazimu kiongozi huyo wa taifa kuagiza chakula cha mchana alichokuwa ameandaliwa kifikishwe mahali alipobarizi, hivyo akala papo hapo.

Punde alipomaliza maakuli, Mzee Kenyatta aliuliza wenyeji jina halisi la mti huo uliomsitiri kwa kivuli chake mwanana.

Alipoambiwa mti huo unaitwa Mpeketo, Mzee Kenyatta alicheka na kisha kuagiza kwamba kuanzia wakati huo eneo hilo zima la Ziwa Mkunguya libadilishwe jina na kulibandika jina la sasa la Mpeketoni.

Hivyo ndivyo Mpeketoni, kaunti ya Lamu ilivyozaliwa kutokana na mapenzi ya Mzee Kenyatta kwa mti wa Mpeketo uliomsitiri.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili mnamo Ijumaa, wazee wa mjini Mpeketoni walieleza hofu kwamba idadi ya mti wa Mpeketo eneo hilo inadimimia kila kukicha.

David Muiga, mmoja wa wazee wa Mpeketoni, alisema wakati umewadia kwa wananchi wa eneo hilo kutengewa siku maalum ya kuutambua na kuupanda kwa wingi mti wa Mpeketo.

Bw Muiga aliutaja mti wa Mpeketo kuwa turathi muhimu kwa jamii ya Mpeketoni na Lamu kwa jumla kutokana na kigezo kwamba ndio uliozaa jina au mji wa ‘Mpeketoni’.

“Awali eneo hili la Lamu Magharibi liliitwa Ziwa Mkunguya kutokana na kuwa mwenyeji wa Ziwa Mkunguya ambalo baadaye liligeuzwa jina na kuitwa Ziwa Kenyatta. Mzee Jomo Kenyatta ndiye aliyeliita eneo hili Mpeketoni kutokana na miti mikubwamikubwa iliyokuwepo ya Mipeketo,” akaeleza Bw Muiga.

Aliongeza, “Na ndio sababu twataka mti wa Mpeketo kutambuliwa kupitia kutengwa kwa siku ya kupanda miti aina hiyo. Twahofia hali ikiendelea hivi huenda mti wa Mpeketo ukaangambia kabisa.”

Paul Mwangi, mkazi wa Mpeketoni, aliwapendekezea madiwani wa Bunge la Kaunti ya Lamu kuibuka na mswada, waujadili na kuupitisha bungeni ili kuwepo na sheria itakayowashurutisha wananchi, hasa wale wanaoishi taarafa ya Mpeketoni na viunga vyake kupanda mipeketo.

Bw Mwangi alisema ni kupitia kuwepo kwa sheria kama hiyo ambapo wananchi watajituma vilivyo kuhakikisha mti wa Mpeketo unapandwa na kuenea kwa wingi Mpeketoni.

“Ni ombi letu kwamba huku sisi kama wazee tukihimiza vijana wetu kuuenzi na kuupanda kwa wingi mti wetu asilia wa Mpeketo, madiwani wetu pia wapitishe sheria bungeni itakayotenga siku maalum ya kupanda mipeketo. Wakifanya hivyo huo mti hautapotea eneo letu kamwe,” akasisitiza Bw Mwangi.

Bi Maru Kariuki, mkazi wa mtaa wa Umoja mjini Mpeketoni, alisema endapo itafikia wakati mti wa Mpeketo uangamie, hilo litamaanisha ni sawa na kuipoteza hadhi ya mji wenyewe wa Mpeketoni.

Bi Kariuki alisema ili kumuenzi hayati Mzee Jomo Kenyatta na mapenzi yake kwa mti wa Mpeketo, itakuwa busara kwa wananchi wa Mpeketoni kuhakikisha wanaongeza idadi ya miti hiyo ya Mpeketo badala ya kuiacha iangamie.

“Mti wa Mpeketo ndio uliozaa jina Mpeketoni. Hivyo ni jambo la busara ikiwa wananchi watajikaza kuongeza idadi ya mipeketo Mpeketoni badala ya kuiacha kuangamia. Miti hiyo ikipotea itamaanisha hadhi ya Mpeketoni pia imeondoka,” akasema Bi Kariuki.

Naye Bw Samuel Karanja aliwahimiza wana Mpeketoni kujikaza kuipanda miti ya mipeketo ili angalau kumbkumbu za hayati Mzee Jomo Kenyatta aliyebandika eneo hilo jina la Mpeketoni zisisahaulike.

Mbali na kuwa na kivuli safi, mti wa Mpeketo pia unasifika kwa kuwa na mbao nzuri.

Wazee pia wanautambua mti huo kuwa dawa ya kipekee kwa wanaoumwa na meno.

“Kwa wanaougua meno kuuma, waweza ukabambua ganda la Mpeketo au kuchimba mizizi yake. Chemsha maganda au mizizi kwenye maji halafu upige funda na kusukutua mdomoni. Maumivu yako ya meno yataangamia papo hapo,” akasema Mzee Ezekiel Muchiri.