Habari za Kitaifa

Serikali yakanusha kumnyima Uhuru haki yake kama Rais Mstaafu

June 10th, 2024 1 min read

NA FATUMA BARIKI

MSEMAJI wa Serikali Isaac Mwaura amepuuzilia mbali taarifa ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwamba amenyimwa haki zake zikiwemo marupurupu kama inavyohitajika kisheria.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyumba vya habari Jumatatu jioni, Serikali kupitia kwa Bw Mwaura inasema imetekeleza matakwa yote ya Bw Kenyatta, ikiwemo kumnunulia magari na kulipa mishahara ya wafanyakazi wake kinyume na alivyodai Msemaji wa Afisi ya Rais Mstaafu, Bi Kanze Dena, awali Jumatatu.

“Tumempa Bw Kenyatta jumla ya magari 14, na kinyume na madai kwamba hayalipiwi mafuta, rekodi zetu zinaonyesha kwamba juzi tu, Mei 15, 2024, magari hayo yalijazwa mafuta kupitia kwa kadi ya State House Master Card,” akasema Bw Mwaura.

Kuhusu madai ya kukataa kumkodishia afisi ya kuendesha shughuli zake kama rais mstaafu, Serikali inasema kwamba lazima Bw Kenyatta akubali kutumia jumba alilotumia aliyekuwa Rais Mstaafu, Hayati Mwai Kibaki kule Nyari.

“Hatuwezi kulipia kodi nyumba ya kibinafsi anayotumia kama ofisi, hiyo ni sawa na kukiuka sheria. Afisi aliyotumia Bw Kibaki kwa miaka tisa bado iko katika hali shwari kabisa na inafaa kwa Rais Mstaafu,” ikaendelea kusema taarifa hiyo.