Habari za Kitaifa

Wafungwa nao pia wafikiwa na mvua ya ushuru gerezani

June 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA DAVID MWERE

KILA mfungwa kwenye jela atapata fursa ya kufanya kazi na kulipa ushuru huku serikali ikishirikiana na wadau husika, wakiwemo, Mpango wa Wakfu wa Chandaria unaolenga kuzindua miradi ya maendeleo kwenye magereza.

Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa maduka ya kuoka keki na kuboresha karakana zilizopo, kati ya shughuli zingine zinazoingiza mapato katika vituo vya kurekebisha tabia nchini.

Hata ingawa hajafichua kiwango cha fedha kitakachotumika kufanikisha mpango huo, Katibu katika Idara ya Magereza, Dkt Salome Beacco, amedokeza kuwa serikali imetambua nguzo nane kuona kwamba mahabusu wanapata mafunzo na kufanya kazi, kabla kuungana na jamii kifungo chao kinapokamilika.

Nguzo hizo zinajumuisha kufufua mashamba ya magereza kuendeleza kilimo, viwanda, taasisi mbalimbali zikiwemo za masomo, sekta ya ujenzi wa nyumba, barabara, mazingira, idara ya sheria, ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki, kati ya nyinginezo.

“Tunataka wafungwa wafanye kazi, walipe ushuru na kusaidia familia zao huku wakiendelea kuhudumu vifungo vyao kubadilisha tabia na mienendo,” Dkt Beacco akasema.

Kwa sasa, serikali inatengeneza maduka ya kuoka keki katika magereza ya Kisumu, Mombasa, Meru, Nyeri na Eldoret.

Kenya, huduma katika Idara ya Magereza zimekuwa zikiimarika, zikiwemo kuboresha mlo, matibabu, malazi, usafiri na malezi kwa wanawake wanaojifungua wakiwa kwenye jela, kupitia uhamasishaji wa maafisa wanaohudumu.

Awali, mahabusu waliokuwa wakishiriki kazi mbalimbali za ujenzi wa taifa walikuwa wakipata ‘mshahara’ japo mpango huo ukadidimia.

Idara ya magereza imekuwa ikishiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kama vile kuunda fanicha, 2012 ikiingia kwenye historia kwa kuboresha vikao vya Bunge la Kitaifa na lile la Seneti, kila moja ikigharimu kima cha Sh400, 000.

Gereza la Kamiti ndilo lenye karakana kubwa zaidi katika uundaji wa bidhaa na vifaa vya mbao.

Kwa sasa, Idara ya Magereza inaendelea kurekebisha Makao Makuu ya Upelelezi wa Uhalifu na Jinai (DCI).

Isitoshe, inaendeleza ukulima kwenye jumla ya ekari zake 8, 000 nchini.

Wafungwa wanatarajiwa kusaidia katika ujenzi wa nyumba 28, 000, chini ya Mpango wa Nyumba za Bei Nafuu.

Kenya, ina jumla ya magereza 135, yenye zaidi ya wafungwa 63, 000.