Wapelelezi wa kifo cha tineja aliyebakwa wapewa makataa
NA MWANGI MUIRURI
MAAFISA wa upelelezi katika Kaunti ya Murang’a ambao wanachunguza kifo cha tineja Beth Wambui aliyepatikana Aprili 7, 2024, akiwa amebakwa, kudungwa kwa kisu na hatimaye kuchomwa na asidi, wamepewa makataa ya kufaulu la sivyo Rais William Ruto aingilie kati.
Makataa hayo yametolewa na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Bi Betty Maina pamoja na Seneta Joe Nyutu.
Baada ya uvamizi huo, Wambui alikaa hospitalini hadi Mei 25, 2024, alipoaga dunia na hatimaye akazikwa Juni 7, 2024.
Katika mazishi hayo, Bi Maina alisoma risala za rambirambi za Rais Ruto ambaye hapo awali alikuwa ametoa mchango wake wa Sh1.5 milioni kupambana na bili ambayo ilikuwa imetinga Sh2.1 milioni.
Risala za Rais zilisema kwamba “nimepokea habari za mauti ya Wambui kwa majonzi makuu kwa kuwa tulikuwa tumejitolea kwa hali na mali kumsaidia kuibuka na ushindi dhidi ya majeraha yake.”
“Alifanyiwa kitendo cha udhalimu ambacho ni sharti utaratibu wa kisheria kufuatwa na vitengo vyetu vya kiusalama, sina shaka, vinajua la kufanya,” akasema Rais Ruto.
Katika hali hiyo, ripoti ya uchunguzi ambayo Taifa Leo iliona, inasema kwamba kuna mambo yanayofuatiliwa.
“Katika kutatua hii kesi, tunachochunguza ni uwezekano kwamba uvamizi huo ulichochewa na tendo la ubakaji kutoka kwa mwanamume aliyefahamika na mwathiriwa na katika hali ya kufunika ujambazi huo, akapanga njama ya kumuoa,” ripoti hiyo ambayo imewasilishwa kwa Kamati ya kiusalama ya Kaunti inayoongozwa na Kamishna Joshua Nkanatha ikasema.
Iliongeza kwamba kichocheo kingine kinachofuatwa ni kuhusu uwezekano wa wasichana kadha kumpigania mwanamume mmoja kiasi cha kuzua wivu wa maangamizi.
Suala jingine linalomulikwa ni kuhusu uwezekano kwamba uvamizi huo ulichochewa tu na ukatili wa utumizi wa dawa za kulevya.
“Pia tunafuatilia uwezekano kwamba uvamizi huo ulichochewa na kisasi huku kukiwa na madai kwamba kuna mmoja wa familia yao ambaye amekuwa akihusishwa na madai ya kuwabaka wasichana wa majirani,” ripoti hiyo ikasema
Babake marehemu, Bw Peter Kirii aliambia Taifa Leo kwamba “kabla ya msichana wangu kuaga dunia, alikuwa amewapa maafisa wa uchunguzi majina ya washukiwa watano ambao walidaiwa kuhusika na ukatili huo”.
“Washukiwa watatu kati ya watano walikamatwa lakini wakaachiliwa huru katika mazingira ambayo hatukufichuliwa,” akasema Bw Kirii.
Mzazi huyo aliongeza kwamba kile wanachotaka kama familia ni washukiwa hao wote wanaswe na “miongoni mwao tujue waliohusika na walioshuhudia”.
Uvamizi huo ulianza kujipa taswira wakati Wambui alifika katika baa moja ya mjini Kenol kuhudhuria sherehe ya mwenzake aliyekuwa akiadhimisha siku ya kuzaliwa.
Wambui alikuwa amekamilisha masomo yake ya Kidato cha Nne mwaka 2023 na alikuwa ameambia wazazi wake kutoka kijiji cha Kangangu kilichoko eneobunge la Maragua kwamba alikuwa ameenda kutembelea rafiki yake wa kike katika mtaa huo wa Kenol.
Lakini safari hiyo ya sherehe iligeuka kuwa masikitiko makuu wakati, mwendo wa saa sita usiku, alipatikana kando ya barabara karibu na kituo cha polisi cha Kabati akiwa na majeraha ya kudungwa mara mbili kwa kisu tumboni na kisha mwili wake kumwagiliwa kemikali iliyomchoma upande wake wa kulia wa kichwa, kifuani na mapaja hadi kwa miguu.
Kando na majeraha hayo, kwenye sikio lake la kushoto na pia kifuani, kulikuwa na alama za kukatika.
Maafisa wa polisi waliofika katika eneo ambapo msichana huyo alikuwa ametupwa walisema katika taarifa yao kwamba walimpata akiwa hali mahututi na wakamkimbiza hadi katika hospitali kuu ya Thika lakini wakapata madaktari wamegoma.
Ndipo alipelekwa hadi hospitali nyingine mbili za kibinafsi lakini akakosa kupokelewa kwa kukosa pesa.
Mamake msichana huyo Bi Esther Njeri aliambia Taifa Leo kwamba “mimi mamake msichana huyu nilisononeka kiasi cha kutojielewa”.
Baada ya kukaa hospitalini kwa zaidi ya mwezi mmoja, Wambui aliaga dunia mnamo Mei 25, 2024, huku akiwa na bili ya Sh2.1 milioni na ambazo kupitia kwa ushirikishi wa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Bi Betty Maina, Rais William Ruto alituma mchango wake wa Sh1.5 milioni.
Katika mazishi ya Wambui yaliyoandaliwa mnamo Juni 7, 2024, katika kijiji cha Karugia kilichoko Kaunti ya Murang’a, Bi Maina alilalamika kwamba “hadi sasa polisi wanazubaa na hakuna mshukiwa ambaye ametiwa mbaroni”.
“Ningetaka kuwaambia maafisa wa polisi kwamba hili sio suala la mzaha na ikiwa hamtamkamata yeyote aliyehusika, basi mjiandae kwa hali ambapo nitamshawishi Rais atoe sauti kuhusu mwendazake na haki yake,” Bi Maina akasema.
Mzazi – Bi Njeri – alisema kwamba “mimi ninaomba serikali ichunguze kisa hiki hadi iwakamate waliohusika”.
“Ningalikuwa na ufunuo kwamba haya yangalimtokea mwanangu ningalikataa atoke nyumbani kwangu siku hiyo na ikiwa ni lazima angalienda, basi mimi ningaliandamana naye hadi kwa hiyo baa bila kujali kwamba mimi nimeokoka katika imani ya Kikristo ndani ya kanisa la Akorino,” akasema Bi Njeri.
Babake marehemu, Bw Kirii, alisema kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuhusu waliohusika na ukatili huo na ni jukumu la maafisa wa polisi kuwanasa na kuwabebesha lawama mahakamani.
Kamanda wa polisi wa Murang’a Bw Kainga Mathiu alisema kwamba kisa hicho kinachunguzwa “na hivi karibuni tutawanasa washukiwa”.
Ni hali ambayo imezua hasira nyingi katika jamii kiasi cha kumfikia Waziri wa Jinsia Bi Aisha Jumwa ambaye ameonya maafisa wa usalama wa Kaunti ya Murang’a kwamba ni lazima wachunguze kisa hicho na waliohusika wakamatwe na wawajibishwe mkondo wa sheria.
“Mimi nimearifiwa kwamba waliohusika katika kisa hicho ni watu wanaojulikana. Ni watu walio na uhusiano wa karibu na mwathiriwa na ningetaka kutoa mwelekeo wa kiserikali kwamba ni lazima wakamatwe na washtakiwe,” akasema Bi Jumwa.