Gachagua awashauri wasanii waache kutumia mihadarati
NA MWANGI MUIRURI
NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewataka wasanii nchini wanaosaka riziki kupitia ubunifu wa kutunga nyimbo na kutengeneza maudhui mengine, wawe wakizingatia maadili ya kijamii hasa kwa kujiepusha na uchafu wa kimawazo ambao hauwezi ukatoa mwelekeo kwa watoto.
Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa msanii Kevin Mbuvi Kioko almaarufu Bahati wa kupeperusha kipindi chake cha The Bahati Empire kwa Netflix, Bw Gachagua aidha aliwataka wasanii waachane na mihadarati akisema imeharibu maisha ya wengi.
The Bahati Empire Reality Show ni mradi ambao utawezesha usanii wake Bahati kuwa na soko la takribani watu 222 milioni kote duniani, hesabu ya wengine ikiwa itakuwa raha iliyoje ikiwa soko hilo tu litakubali kumpa msanii huyo angalau Sh10 pekee kutoka kwa kila mmojawapo.
Bw Gachagua aliwataka wasanii wajue kwamba akili zao zinahitaji kuwa safi bila ushawishi wa mihadarati. Akiwakumbusha kwamba katika enzi zake, alikuwa moto wa kuotea mbali katika masuala ya usanii.
“Badala ya kujiingiza kwa matumizi ya mihadarati, muwe katika mstari wa mbele kutoa vipindi ambavyo vitaangazia hasara kubwa ya mihadarati katika jamii,” akasema Bw Gachagua.
Pia, aliwataka wasanii wajue kwamba sawa na wanasiasa, jinsi wapandavyo ngazi ya ufanisi, kutazuka maadui wa kuwavunja roho kupitia ukatili mitandaoni. Alisema kwamba hao hufahamika kama ‘kamati ya roho chafu’.
“Nawaibia siri. Kwetu katika jamii ya Agikuyu, kuna msemo kwamba mti usio na matunda hauwezi ukarushiwa mawe na wapita njia. Ukiwa na matunda ya ufanisi ni lazima urushiwe mawe. Dawa ya kustahimili mipigo ni kukosa kuzingatia hao wa wivu na kinyongo na usiwe wa kujali wanasema nini kukuhusu. Wapuuze,” akashauri.
Aliwataka wasanii wamuige yeye mwenyewe kwa kuwa “ningezingatia hao wakatili wa mitandaoni, nisingefanikiwa kuibuka kuwa Naibu Rais”.
“Mimi ni mfano wa kejeli kupitia mitandao na mikutano ya kisiasa kiasi kwamba hata walisema sijui Kizungu,” akasema.
Lakini alisema kwamba yeye alizingatia kujinoa tu hadi wakati wa mdahalo wa wawaniaji wenza wa wagombea wa urais mwaka 2022.
Bw Gachagua alimenyana na Bi Martha Karua wa upande wa Azimio La Umoja-One Kenya.
“Ni hapo ndipo walielewa Kizungu changu. Pia walisema sijui kuvaa nguo… nione nilivyopiga luku kwa sasa,” akasema.
Alisema ulimwengu uko na watu walio na wivu na kinyongo “na hata sasa wananiita mkabila kwa kuwa nimesema ninataka kuunganisha watu wa jamii yangu”.
Bw Gachagua aliwaambia wasanii kwamba “ninyi hamnijui vizuri… mimi ni shabiki wenu sugu hasa katika safu ya muziki kwa kuwa ngoma hupapasa roho yangu hadi kuipa utulivu wa ajabu”.
Alikiri kwamba muziki wa Jackson Ngechu Makini almaarufu CMB Prezzo, humpagawisha.
Aliwataka wasanii wajue kwamba wakati wanaunda pesa kupitia usanii wao wasije wakapotoshwa kwamba hali hiyo itadumu.
“Pesa ni tamu na ni nzuri… Hasa sisi watu wa kutoka eneo la Mlima Kenya tumekuwa tukisutwa kwamba mapenzi yetu kwa pesa yako juu sana. Lakini jamii nyingi nchini nazo zimeingia katika mazoea ya kupenda pesa. Lakini ningetaka muelewe kwamba pesa ni bure ikiwa utazipata kisha zikakosa kukupa uthabiti wakati wa uzeeni,” akasema.
Aliwataka wasanii waelewe kwamba siku moja, watazeeka na wawe hawana uwezo wa kuunda pesa kupitia hali yoyote ile.
“Nawaomba muwekeze pesa ambazo mnapata mkiwa bado barobaro. Ningetaka muige huyu msanii mwenzenu ambaye ni Bahati. Yeye kwa pato lake, ameweza kujengea familia yake ya watoto watano boma la kifahari. Ninawasihi wasanii wote walio kwa pato kwa sasa wazingatie kumiliki maboma yao ili malandilondi wakome kuwasumbua kila tarehe tano ya kila mwezi,” akasema.
Aliwataka wasanii wajinunulie ploti na wajenge nyumba ili wakizeeka, wawe wakiringia watoto wao na wajukuu kwamba “wakati wa ujana wangu na nilipokuwa maarufu katika mitandao ya kijamii, niliwajengea hizi nyumba”.
Aliwataka wasanii wakishafanikiwa wawe na roho ya upendo na wawe wakisaidia jamii iliyowapa nafasi ya kupaa.
“Hii ndio sababu namfagilia Bahati kwa kuwa baada ya kufanikiwa, amechukua mtoto yatima na kumpa makao kwake nyumbani kama wa familia yake. Hongera sana. Wengi wako na mazoea ya kusahau safari yao ya kupanda juu na wakishafika, hawawezi wakawashika wengine mikono,” akasema kiongozi huyo.