Wizara yaanza kutafuta watoto waliokosa chanjo ambayo sasa imewasili
WIZARA ya Afya imeanza kuwasaka watoto ambao walikosa chanjo iliyotolewa miezi miwili iliyopita, baada ya kuletwa kwa chanjo milioni nane nchini wiki jana.
Serikali imewataka wazazi wafike katika vituo vya afya ili watoto wao wapokee chanjo walizokosa.
Wizara inalenga kuwatumia wahudumu wa afya nyanjani kuwapata watoto waliokosa chanjo hiyo muhimu iliyokuwa imeisha nchini ili wahudumiwe.
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha jana alisema kuwa serikali itahakikisha hakuna mtoto ambaye anakosa chanjo baada ya kufanikiwa kuisafirisha nchini.
Zaidi ya watoto 300,000 kote nchini wanalengwa kupewa chanjo hiyo, idadi hiyo ikiwakilisha asilimia 18 ya watoto milioni 1.6 ambao huipokea kila mwaka kulingana na wizara ya afya.
Bi Nakhumicha amewaamrisha wahudumu wote wa afya katika kaunti mbalimbali wahakikishe watoto ambao hawakuchanjwa, wanawajibikiwa mara hii.
“Mambo hayakupaswa kutokea jinsi yalivyofanyika lakini hali sasa imedhibitiwa. Sasa tunakazana kuhakikisha kuwa watoto wote wamepewa chanjo,” akasema Bi Nakhumicha akiwa Kitale.
Waziri huyo alisema wizara yake inashirikiana na serikali za kaunti kuwafikia wazazi ambao watoto wao walikosa chanjo hiyo.
Alisema kukosekana kwa chanjo hiyo kulitokana na kampuni inayoiwasilisha kwa serikali kukosa kulipwa deni lake.
“Mchakato wa kulipa Kampuni ya kutengeneza chanjo Gavin na Shirika la Kimataifa la UNICEF unaendelea. Sehemu ya deni hilo ililipwa wiki jana na sasa tunachangamkia utoaji wa zabuni ya mapema kuhakikisha kuwa chanjo hiyo haiadimiki tena nchini,” akaongeza.
Mama Josefina Wasike ambaye mtoto wake alikosa chanjo hiyo alisema alilemewa na gharama za kumpeleka hospitali ya kibinafsi na anafurahi kuwa sasa atahudumiwa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa Trans Nzoia Sam Ojwang’, bado wanasubiri wasambaziwe chanjo hiyo inayosafirishwa kwenye makontena spesheli yenye majokofu.
“Kama tu kaunti nyingine, hatujaipata chanjo hiyo. Bado tunasubiri lakini serikali kuu imetuhakikishia kuwa chanjo itafika kwetu hivi karibuni,” akasema Bw Ojwang’.
Bi Nakhumicha alisema kuwa serikali pia inamakinika kuhakikisha raia wanapata huduma bora za kiafya siku zijazo.
“Kuanzia Julai, Wakenya watakuwa na nafasi ya kujisajili kwa Mamlaka ya Afya ya Kijamii ambayo itawapa bima ya kimatibabu tena kwa bei nafuu,” akasema.