Maoni

Tofauti za Ruto na Gachagua ni za maslahi yao wala si wakazi wa Mlima Kenya

June 12th, 2024 1 min read

Na BENSON MATHEKA

KUMEKUWA na mjadala mkali kuhusu uhusiano wa Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua huku mirengo miwili ikiibuka.

Kilichojitokeza katika mdahalo huo ambao ninaamini utaendelea ni kwamba Bw Gachagua anapigwa vita ndani ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) na katika muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Anaonekana kuwa katika hali ngumu huku wanasiasa chipukizi kutoka ngome yake ya Mlima Kenya wakimkosoa vikali hasa kwa kuunga mbinu ya ugavi wa mapato kwa kutegemea idadi ya watu.

Rais William Ruto alinyamaza mdahalo huo ulipokuwa ukiendelea hadi juzi alipoonekana kusimama na Gachagua.

Kulingana na Rais, ni yeye aliyemchagua Gachagua kuwa naibu wake na atafanya kazi naye.

Hapa alichomaanisha rais, ni kuwa hakuna njia anayoweza kumpokonya Gachagua wadhifa wake isipokuwa kwa kurai na kufadhili wabunge kuwasilisha hoja ya kumuondoa ofisini.

Changamoto

Pili, anajua ni mapema sana kuonyesha kuwa ndoa yake na Gachagua imeingia doa.

Gachagua naye amegundua kuwa bila eneo la Mlima Kenya kuwa na umoja, atakuwa na kibarua kizito kuwa mgombea mwenza wa Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

Hivyo basi, wanachofanya viongozi hao wawili kwa kuonekana kupuuza mpasuko kati yao ni maslahi yao ya kibinafsi.

Gachagua anataka kuokoa hatima yake ya kisiasa kabla ya 2027 na anafanya hivyo kwa kuonyesha kuwa anajali umoja wa Mlima Kenya aliochangia kusambaratisha kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 ili kulinda maslahi yake wakati huo.

Ruto naye anataka kulinda maslahi yake ya sasa aliyopata kwa kugawanya Mlima Kenya wakati huu hadi akafaulu kuwa rais.

Hivyo basi, kila hatua anayochukua mwanasiasa huwa ni ya kutimiza maslahi yake ya kibinafsi na sio kufaidi wakazi anaoonekana au kudai kuwakilisha.